Habari Mseto

KCSE: Wavulana wengi kujiunga na vyuo vikuu

December 22nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAVULANA 16, 127 zaidi ya wasichana watajiunga na vyuo vikuu mwaka 2019 kulingana na matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) yaliyotangazwa Ijumaa.

Hii ni kwa sababu idadi ya wavulana waliopata gredi ya C+ kwenda juu ilizidi ile ya wenzao wa kike.

Katika orodha ya wanafunzi 100 bora, kuna wavulana 64 na wasichana 36. Hii ina maana kuwa kuna wavulana 28 zaidi.

Na katika wanafunzi 20 bora, 14 ni wavulana huku sita wakiwa wasichana.

Matokeo hayo, yaliyotolewa rasmi na Waziri wa Elimu Amina Mohamed katika makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), yalimaanisha kuwa katika miaka mitatu mfululizo wavulana 11,000, kwa wastani, wamekuwa wakijiunga na vyuo vikuu kuliko wasichana.

Mwaka huu pekee idadi ya wavulana walipata gredi ya C+ kwenda juu ilikuwa 53,252 ikilinganishwa na wasichana 38,514.

Kwa misingi ya matokeo katika kila somo, wasichana waliwashinda wavulana katika masomo sita kati ya masomo 26.

“Watahiniwa wasichana walifanya vizuri kuliko wavulana katika masomo kama vile Kiingereza, Kiswahili, Dini, Sayansi Kimu (Home Science), Sanaa na Muundo na Somo la Uhunzi (Metal Work),” akasema Waziri Mohamed.

Kutajwa kwa somo la uhunzi, ambayo ni somo la utendaji unaotarajiwa wavulana kufanya vizuri, kuliwachangamsha waliohudhuria shughuli hiyo ya kutangazwa kwa matokeo ya KCSE.

“Matokeo ya wasichana katika somo la uhunzi yalinipa tabasamu ya kipekee. Nadhana sisi kama jinsia ya kike tunaelekea kuwafikia wanaume,” akasema Waziri huku akishangiliwa.

Kwa misingi ya wanafunzi waliojisajili kwa KCSE mwaka huu, idadi ya wasichana inaendelea kukaribia ile ya wavulana katika miaka mitatu iliyopita.

Mnamo 2016 kulikuwa na wavulana 27,865 kuliko wasichana. Idadi hiyo ilipungua hadi kufikia 19,308 mwaka 2017.

Na mwaka huu, idadi hiyo imepungua zaidi hadi kufikia 17,052. Hii ni kwa sababu wavulana 321,576 walifanya mtihani huo ikilinganishwa na wasichana 321,576.