Makala

KDF anayesherehekea Leba Dei akichuuza maji kwa mkokoteni asimulia alivyoiletea Kenya sifa

April 30th, 2018 2 min read

NA PETER MBURU

HUKU Wakenya wakisubiri kusherehekea siku ya wafanyakazi ya ‘Leba dei’ miaka 55 tangu nchi kupata Uhuru Jumanne, kwa Christopher Kariuki, ni kumbukumbu za siku alizoisherehekea siku hiyo kutoka moyoni tu zilizomjaa akilini.

Bw Kariuki, 60, ameisherehekea siku hii kwa ngazi tofauti; kwanza aliwahi kuwa afisa wa jeshi (KDF) na pia bingwa wa ndondi maarufu kwa miaka mingi kiasi cha kuiwakilisha Kenya kwenye mashindano kadha.

Hata hivyo, kesho mzee huyo anaishi kwa kumbukumbu tu kwani sasa kazi yake kuu na ambayo ataisherehekea ni ile aifanyayo ya kuuza maji, mawe na kuwahamisha watu kwa kutumia mikokoteni kwenye mtaa wa Kivumbini, Nakuru.

Bw Kariuki, almaarufu ‘Kawasaki’ sasa anafanya kazi hiyo ya sulubu licha ya umri wake mkubwa na huduma alizowahi kulipa taifa hili, ili kuendeleza maisha yake.

Bondia wa zamani Christopher Kariuki aonyesha makali yake katika ndondi. Picha/ Peter Mburu

Alipotembelewa na Taifa Leo, mzee huyo alikuwa mwingi wa furaha huku kumbukumbu za maisha yake ya ujana zikimjaa akilini.

“Nimetoa huduma nyingi kwa taifa hili na kuliwakilisha mara nyingi. Nilifanya kazi kama afisa wa KDF na pia kuiwakilisha Kenya kwa michezo ya masumbwi kwa miaka mingi ambapo nilishindia Kenya mataji na kuvuta heshima,” Bw Kariuki akaeleza Taifa Leo.

Ni katika miaka yake ya kucheza ndondi akiwa jeshini ndipo alipata jina la majazi ‘Kawasaki’ kutokana na kasi yake ya kurusha makonde na kuwatia adabu mahasimu.

“Nilijiunga na jeshi mwaka wa 1977 na mara moja nikaanza kushiriki mchezo wa ndondi, baadaye nilipata umaarufu kutokana na kurekodi matokeo mema na nikaishia kuwa bingwa na kupata mataji ya mchezaji bora kwa miaka mingi,” Bw Kariuki akaeleza.

Bw Kariuki alieleza kuwa alikuwa kwenye kikosi cha 1st Batallion kituo cha Nanyuki Airbase na kulingana naye, hadi alipojiuzulu kazi hiyo mwaka wa 1984, alikuwa ameiwakilisha Kenya kwa mashindano mengi katika mataifa ya nje kama Bangkok na Uganda na kurudi na mataji.

Mwanamasumbwi mtajika Christopher Kariuki aonyesha mojawapo ya mataji aliyoshinda baada ya kuwaangusha washindani. Picha/ Peter Mburu

Weledi wa masumbwi

“Nilikuwa ‘mambo mbaya’ katika mchezo huo, ningepigana Kenya kisha kuiwakilisha nchi nje na kurudi na mataji mzo mzo. Aidha, nilishiriki mashindano kati ya vikosi vya kijeshi ambapo nilikuwa bingwa,” anakumbuka mzee huyo, akijutia maisha anayoishi sasa ambayo hakuyaotea siku hizo kwani nyota yake iling’aa.

Kwa sasa, unapofika eneo lake la kazi, kinachokupiga machoni mwanzo ni mikokoteni mingi atumiayo kuuzia maji na kuwafunza wakazi wa mtaa huo akitumia mawe magumu yakiwa kwenye magunia.

Utampata na sare yake rasmi ikiwa aproni ya manjano pamoja na wafanyakazi wake wawili, wote wakifanya juhudi kupata riziki ya siku.

“Hivi ndinvyo maisha yaligeuka, sasa lazima nijitume ili kuweka chakula mezani. Sina uhakika kama kuna mwanajeshi ama mwanamasumbwi yeyote nchini atakuwa na ujasiri wa kufanya kazi ya aina hii lakini mimi sina budi,” bingwa wa zamani akaeleza Taifa Leo.

‘Kawasaki’ aonyesha taji na mojawapo ya picha alizopigwa akimlima hasimu kwenye pambano la mwaka wa 1981. Picha/ Peter Mburu

Chumba cha mabati

Nyumbani kwake mambo si tofauti kwani anaishi kwenye chumba cha mabati pamoja na mkewe wa zaidi ya miaka 40 Bi Grace Wahu Kariuki. Hata hivyo, licha ya maisha yao ya uchochole ya sasa, wanandoa hao wanaishi kwa furaha, wakila kile kidogo anachowabariki nacho mwenyezi Mungu.

Vikombe alivyowahi kujishindia pamoja na picha za kumbukumbu sasa ni sumaku ya vumbi inayoashiria wingi wa miaka vilivyoishi humo.

“Kazi yangu sasa ni kuzunguka katika maeneo ambapo majengo yamebomolewa na kuokota mawe haribifu yanayotolewa aina ya hard core, kisha kuwauzia wakazi wanaotaka kukarabati nyumba zao ama vijibarabara,” Bw Kariuki akaeleza.

Ni maisha na kazi hiyo ambayo Bw Kariuki sasa atasherehekea kama mfanyakazi, huku nayo mawazo yakizidi kumzonga na kumkumbusha enzi ambazo nyota yake iling’aa.

“Niliiwakilisha Kenya mara nyingi hata kama sikupewa pesa na zawadi lakini moyoni nilihisi kuridhika, ni maombi yangu kuwa serikali inafaa kunikumbuka pamoja na wenzangu wengi ambao waliwahi kuihudumia nchi kwa kujitolea,” akasema Bw Kariuki.