KDF yafichua ilivyoteka Kismayu na Al-Shabaab

KDF yafichua ilivyoteka Kismayu na Al-Shabaab

NA WACHIRA MWANGI

KITENGO maalum cha boti katika Kikosi cha Jeshi la Wanamaji chenye makao yake Mtongwe, Kaunti ya Mombasa, kilichangia pakubwa kuikomboa Kismayu kutoka kwenye nira za wanamgambo wa Al-Shabaab.al

Tangu 2011, wakati Jeshi la Kenya Defence Forces (KDF) lilipozindua oparesheni Linda Nchi, wanajeshi kadhaa wenye ujuzi katika oparesheni za nchi kavu, anga na majini, walitumwa Somalia.

Naibu Kamanda wa Kikosi Maalum cha Oparesheni katika Jeshi la Wanamaji, Meja Eric Wambugu, aliyekuwa sehemu ya Kitengo cha Boti Maalum (SBU), anasimulia wajibu wao na waliyopitia wakati wa oparesheni hiyo.

Wambugu anaeleza kwamba Jeshi la Wanamaji lilipewa jukumu la kuhakikisha eneo la majini Kenya limelindwa kwa kukabiliana na maadui.

‘Tunapofanya oparesheni ya pamoja, huwa tunaruhusu kila kitengo kuelezea uwezo wao, huwa tunakipa kila kikosi jukumu lake,” asema Meja Wambugu.

SBU ni kitengo mahsusi cha Jeshi la Wanamaji Nchini, ambapo wanajeshi katika kitengo hiki walipokea mafunzo Amerika na Lamu pamoja na US Naval Seal.

Kikosi hiki kilipokea mafunzo maalum katika matibabu ya vitani, safari, kushughulikia meli, ujuzi kuhusu silaha na utaratibu wa kuabiri meli.

Wana maarifa kuhusu kutua kwenye fuo za baharini, husaidia kwa kuimarisha juhudi za Kenya Navy na vitengo vingine katika kushika doria kama jukumu la kimsingi kwenye bandari za Kilindini, Lamu na Shimoni.

‘Huwa tunahakikisha tunaabiri chombo, tunasaka na kukamata chombo chochote kinachotiliwa shaka. Tukidokezewa au tukikumbana na chombo tunachotilia shaka au tunacholenga, wakati tunaposhika doria, tuna utaratibu wa kuhoji, kuabiri na kukipekua,” alisema.

Wajibu mwingine wa kikosi hicho ulikuwa kufahamisha vikosi vingine vya jeshi kuhusu tishio lolote linaloibuka huku kikihakikisha hakuna uhalifu wowote wa majini unaotekelezwa katika maeneo ya majini Kenya.

Vikosi vya SBU kwa kawaida huwa kwenye maji yenye kina kifupi kwenye mikoko ambapo meli haziwezi kwenda na huwa vinakabiliana na uhalifu wa majini, ugaidi, uvuvi haramu na ulanguzi wa bidhaa.

“Vikiwa nyumbani, vitengo hivyo vilipewa mafunzo na kufahamishwa kuhusu mbinu na oparesheni zote na haya yalitusaidia kukamilisha jukumu hilo kama shirika la pamoja katika Maji ya Kenya.

“Wakati huo, mimi binafsi nilitumwa kama afisa wa boti. Nilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba meli zetu zilikuwa zikiendelea na oparesheni asilimia 100. Tulihakikisha vifaa vilidumishwa vyema. Tulihakikisha kwamba jeshi lenye utaalam kuhusu vikosi vya nchi kavu, vilifahamu kuhusu oparesheni za majini,” alisema.

Katika siku hiyo ya uzinduzi wakati meli ndogo zilikuwa zikianza kutuma vikosi maalum kwenda kutua fuoni, SBUs zilikuwa zinashika doria kwenye fuo ili kutoa ulinzi kwa vikosi hivyo.’

Tulidumisha usalama kwa vikosi viliovyokuwa vikitua na pia kukaa chonjo ili kukabiliana na shambulizi lolote ambalo lingetokea,” Meja Wambugu alieleza Taifa Leo.

Meja Wambugu alisema kuwa walipitia matukio yaliyojitokeza zaidi kama fursa. “Tulikabiliwa na changamoto katika kukaribisha wanajeshi wa nchi kavu na vikosi maalum vya kijeshi kuja kufanya oparesheni nasi. Walikuwa wamezoea oparesheni za ardhini na hapa kulikuwa na oparesheni ya majini,” alifafanua.

Alisema walilazimika kuhakikisha kwamba wanajeshi hao walikuwa tayari kufanya oparesheni katika mazingira ya majini. Suala jingine lililojitokeza kama changamoto lilikuwa kupakua vifaa vya wanajeshi kutoka kwenye meli na kuzipakia katika meli ndogo kutokana na mawimbi makubwa na bahari kuchafuka.

Major Wambugu alieleza kuwa kulainisha mawasiliano miongoni mwa Jeshi la Wanamaji, Vikosi Maalum vya Kijeshi na Jeshi la Anga, ilikuwa changamoto vilevile.

“Unahitaji kuhakikisha kuwa mawasiliano hayavuji kwa adui. Kulainisha mawasiliano yote kutoka kwenye meli hadi vyombo vya angani, jeshi na vitengo maalum vya meli ilikuwa changamoto lakini tulimudu,” akasema Meja Wambugu.

You can share this post!

Presha kwa Solskjaer miti ya Man-Utd ikizidi kuteleza

DOUGLAS MUTUA: Kenya isikubali kutishwa na Somalia

F M