KDF kusaidia kukabiliana na ukame

KDF kusaidia kukabiliana na ukame

Na FLORAH KOECH

MAAFISA wa jeshi la ulinzi nchini (KDF) watashiriki katika mipango ya kukabiliana na makali ya ukame kwa kuchimba visima na kusafirisha maji katika kaunti zinazoathirika na janga hilo.

Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa, alisema kando na usambazaji wa chakula cha msaada kwa wakazi katika kaunti zilizoathirika, hatua hii itazuia vifo vya watu na mifugo.

Alisema hayo Ijumaa alipozuru eneo la Chemoril katika kaunti ndogo ya Tiaty kuongoza shughuli za usambazaji wa chakula cha msaada.

Bw Wamalwa aliongeza kuwa serikali imetenga Sh2 bilioni kufadhili mipango ya kukabiliana na makali ya ukame ambayo ilitangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa janga la kitaifa.

“Hata hivyo, suluhu la kudumu kwa changamoto hii ni kuhakikisha kuwa miradi ya uzalishaji chakula inaanzishwa katika maeneo yanayokabiliwa na hatari ya kukumbwa na ukame kila mwaka. Hii itahakikisha kuwa miradi ya kilimo cha unyunyiziaji inaanzishwa katika maeneo hayo. Jamii za wafugaji katika maeneo hayo zinafaa kusaidiwa zikumbatie kilimo cha mimea ya vyakula,” akasema Bw Wamalwa.

Aliongeza kuwa serikali pia itaendeleza mpango wa kununua mifugo walioathiriwa na ukame ili kuwakinga kutokana na hasara kutokana na ukosefu wa lishe.

“Ufugaji ni kitega uchumi kikuu kwa jamii za wafugaji na serikali imejitolea kuhakikisha kuwa wafugaji hawa hawapati hasara baada ya mifugo wao kufa kwa kukosa maji na lishe. Chini ya mpango huu, wafugaji watauza mifugo wao kwa serikali nyakati za ukame kisha kununua mifugo wengine msimu wa mvua ukianza,” Bw Wamalwa akaongeza.

Waziri aliongeza kuwa serikali kuu inaendeleza mpango wa kutoa fedha kwa familia zilizoathirika na ukame ili ziweze kujikimu.

“Kando na chakula cha msaada, tunapaswa kuwezesha maeneo kame kujitosheleza kwa vyakula badala ya kutoa misaada kila mwaka. Hatua hii pia itazuia mpango wa sasa ambapo tunatoa msaada ya Sh5,400 kwa kila familia katika kaunti zilizoathirika na ukame,” Bw Wamalwa akaeleza.

Alisema kaunti kame kama vile Garissa, Tana River, Samburu na Isiolo tayari zimefaidi kutoka na mpango wa utoaji fedha za kujikimu kwa familia.

Mbunge wa Tiaty William Kamket hata hivyo alilalamika kuwa Kaunti ya Baringo ni mojawapo ya zile zilizoathirika na ukame lakini haijajumuishwa katika orodha ya kaunti zinazopewa fedha za kujikimu.

“Baringo pia inafaa kujumuishwa katika mpango huu wa utoaji Sh5,400 kila mwezi kwa kila familia. Maelfu ya wakazi hapa wameathirika na ukame,” akaeleza.

You can share this post!

Washirika wa Ruto wapuuza chama kipya cha Lonyangapuo

UNESCO kufanya ushirikiano na vyuo vikuu viwili nchini