KDF kusaka sare zilizo mikononi mwa raia

KDF kusaka sare zilizo mikononi mwa raia

Na JOSEPH NDUNDA

Idara ya Jeshi nchini (KDF) inachunguza mauzo ya sare zake kwa umma kati ya Januari mwaka jana na Julai mwaka huu, shughuli haramu inayodaiwa kuendelezwa na baadhi ya maafisa ambao walijipatia Sh500,000.

KDF inashuku wanajeshi hao wamekuwa wakihusika na tabia hiyo inayokiuka kanuni za kijeshi ndipo wakapata pesa hizo kwa muda wa miezi 18 iliyopita.

Koplo Collins Alulu jana aliwasilisha kesi katika mahakama ya Kibera akisema kuwa, wanajeshi waliohusika walipata pesa hizo kisha kuzigawanya kupitia M-pesa.

Kwa hivyo, jeshi lilipata idhini ya korti ili kuchunguza akaunti mbili za benki ya Cooperative ambazo zinadaiwa zilitumika kulipia sare hizo. Pia mawasiliano kwenye simu za baadhi ya wanajeshi wanaodaiwa kuhusika yanachunguzwa kwa lengo la kuwanasa.

“Uchunguzi umeonyesha kuwa, maafisa ambao wamekuwa wakichunguzwa walitumia simu zao kuwasiliana na raia kisha kuiba sare na kuziuza. Inaaminika kuwa baadaye waligawana pesa hizo kupitia M-pesa,” likasema ombi la KDF kwa mahakama.

Kando na sare, vifaa vingine vya kijeshi ambavyo havifai kutumiwa na raia ni pingu na ngao/nembo ya taifa kati ya nyinginezo.

“Ili kuhakikisha uchunguzi unafanikiwa na maafisa waliohusika wananyakwa, ni vyema kwamba kupitia idhini ya korti turuhusiwe kuchunguza akaunti hizo za benki za washukiwa,” likasema ombi lao kwa korti.

Hakimu Mkuu Mkazi wa Kibera Sharon Maroro alikubali ombi hilo la Koplo Alulu ambaye alipewa idhini na makao makuu ya jeshi (D.O.D) kuchunguza suala hilo.

Korti ilimruhusu achunguze taarifa za kifedha za akaunti hizo mbili ya benki ya Co-operative na jinsi zilivyosajiliwa.Uchunguzi huo ulianza baada ya Wizara ya Ulinzi kulalamika kuhusu mauzo ya sare za jeshi kwa raia.

You can share this post!

Dalili Kingi atafuta makao mapya OKA

Wauguzi wagomea chanjo ya corona licha ya amri kali