Habari za Kitaifa

KDF, polisi waliopigana kwenye feri kuadhibiwa

April 30th, 2024 2 min read

NA KEVIN MUTAI

HATUA za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na maafisa wa Polisi ambao watabainika kuwa walikiuka maadili yao baada ya kunaswa kwenye video wakipigana kwenye kivuko cha feri Likoni mjini Mombasa.

Uamuzi huu ulitolewa baada ya kikao kilichoitishwa na kamati ya usalama ya Kaunti Ndogo ya Likoni mnamo Aprili 29, ambacho kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka KDF na Idara ya Kitaifa ya Polisi (NPS), kushughulikia makabiliano yaliyotokea Jumamosi kati ya maafisa wa pande hizo mbili za kiusalama.

“Hatutaki utovu wa nidhamu miongoni mwa maafisa, tunafanyia kazi serikali moja na kwa hivyo tunafaa daima kutetea uhusiano mwema kati ya pande zote mbili,” Naibu Kamishna wa Kaunti ya Likoni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya Kaunti Ndogo ya Likoni, Bw Mwangi Wambugu, aliiambia Nation katika mahojiano.

Kando na Bw Wambugu, waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na afisa mkuu wa Kambi ya Jeshi la Wanamaji ya Mtongwe, Luteni Kanali John Mutabari, kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Likoni, Bw Geoffrey Ruheni, na mkuu wa usalama katika Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), Bw Tony Kibwana.

Wengine waliohudhuria ni wawakilishi kutoka Idara ya Huduma za Feri ya Kenya, maafisa kutoka Idara ya Kitaifa ya Ujasusi na wale wa asasi nyingine za usalama.

Iliamuliwa kuwa, polisi wa kijeshi na NPS wafanye uchunguzi huru kuhusu tukio hilo, kisha watatathmini taarifa zote zitakazokusanywa na kupendekeza hatua zinazofaa dhidi ya wale wanaopatikana na hatia yoyote.

Maafisa wakuu kutoka vitengo vyote viwili vya usalama walikutana katika makao makuu ya feri, ili kwanza kuweka mapatano kati ya vitengo hivyo viwili na kubaini ni nini kilizua ghadhabu iliyosababisha makabiliano.

Makabiliano yasababishwa na kutoelewana

Kulingana na Bw Wambugu, uchunguzi wa awali umegundua kuwa makabiliano hayo yalisababishwa na kutoelewana kati ya maafisa wa polisi wanaosimamia kituo hicho na askari wa KDF.

Wakati huo, maafisa hao wa kijeshi walikuwa wamefika eneo la Likoni na kutaka kupenya kwa nguvu kwenye njia inayoelekea kuabiri feri, jambo lililozua kutoelewana kati yao, walinzi wa kibinafsi wa feri na maafisa wa polisi wanaosimamia kivuko hicho.

“Kulikuwa na mtafaruku wa mawasiliano na lengo letu kuu lilikuwa kutafuta suluhu ya kuhakikisha kuwa hali hiyo haitokei tena. Tulijadili masuala ya ushirikiano ili kuhakikisha kwamba kwenda mbele, mashirika yote ya usalama yanashirikiana kwa pamoja,” akasema Bw Wambugu.

Baada ya kikao chao cha faragha, timu ya maridhiano iliwatembelea maafisa wa usalama katika kivuko ambapo uongozi kutoka Kambi ya Jeshi la Wanamaji la Kenya huko Mtongwe na Huduma ya Polisi ya Kitaifa waliomba radhi, wakiahidi kurejesha amani na utulivu.

Ugomvi huo wa Jumamosi ulizua wasiwasi miongoni mwa umma, likiwa ni tukio la tatu ambapo maafisa wa KDF na polisi wamehusika katika mzozo wa hadharani ndani ya wiki mbili.

Tukio sawia lilikuwa limeripotiwa awali Turkana na jingine kaunti ya Kilifi.