KDF wadaiwa kutesa wananchi barabarani

KDF wadaiwa kutesa wananchi barabarani

Na KALUME KAZUNGU

WANAJESHI wa Kenya (KDF) wamekashifiwa vikali kwa kuendeleza madhila na ukiukaji wa haki za binadamu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Hii ni kufuatia kisa cha wikendi ambapo madereva karibu 30 na utingo wao walidai kusimamishwa na maafisa hao wa KDF na kupigwa kabla ya kulazimishwa kuogelea kwenye dimbwi la tope.

Matukio hayo yalifanyika Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwenye kona ya Nyongoro, kilomita chache baada ya kutoka kizuizi cha polisi cha Gamba kwenye barabara hiyo ya Lamu-Witu-Garsen.Baadhi ya madereva waathiriwa waliohojiwa na Taifa Leo walisema mbali na kuogelea kwenye kidimwi cha maji machafu, wanajeshi pia waliwalazimisha kupakana tope mwili mzima kabla ya kuwaamuru kuingia kwenye magari yao na kurudi walikotoka.

Haya ni licha ya Msemaji wa KDF, Bi Esther Wanjiku kukana vikali kuhusika kwa wanajeshi kwenye matukio hayo. “Kuna vitengo vingi vya usalama vinavyohudumu eneo hilo la Nyongoro lakini KDF hawapo hapo. Sisi hatujahusika kivyovyote kwenye madai hayo ya kupiga madereva na kuwafanya kuogelea kwenye maji machafu,” akasema kanali Wanjiku.

Bw Abdulrazak Abdulrahman ambaye ni dereva wa Bunge la Kaunti ya Lamu alikuwa amewasafirisha baadhi ya madiwani wa Lamu kuhudhuria mkutano mjini Mombasa na alikuwa barabarani kurudi Lamu kabla ya kukumbana na maafisa hao.

“Nilitoka Mombasa majira ya saa nne usiku. Nilifika Minjila na Gamba mwendo wa saa kumi unusu. Baada ya kukaguliwa na walinda usalama pale, niliruhusiwa kuendelea na safari yangu.“Tulikuwa madereva kadhaa wa malori na magari mengine.

Tulipofika Nyongoro tulisimamishwa na wanajeshi ambao walituamuru kushuka na kisha kutupeleka kwenye kidimbwi cha maji machafu na kutulazimisha tuogelee pale,” akasema Bw Abdulrahaman. Bw Al-amin Nasai ambaye ni dereva wa lori alidai kuwa maafisa hao waliwapiga kwa mtutu wa bunduki na kuwaacha wengine wakiwa na majeraha mabaya.

Bw Nasai anasema walikalishwa kwenye tope na kulazimishwa kuogelea kwa zaidi ya nusu saa kabla ya kuamriwa warudi kwenye magari yao na kurudi walikotoka.“Niko na shida ya macho. Hutumia miwani. Siku hiyo miwani yangu iliharibiwa na hao wanajeshi.

Kwa sasa miwani sina. Si haki tulivyofanyiwa,” akasema Bw Nasai.Bw Ali Paraza Omar ambaye pia ni dereva wa lori la kubeba mizigo linalohudumu kwenye barabara ya Lamu-Mombasa aliiomba serikali kuweka wazi iwapo marufuku ya kusafiri usiku kwa magari ya mizigo ni kweli imeondolewa kwenye barabara hiyoi au la.

Juma lililopita, Kamishna wa eneo la Pwani, Bw John Elungata alitangaza kuondolewa kwa marufuku ua kusafiri usiku kwa magari ya abiria kwenye barabara ya Lamu-Witu-Garsen.“Tunavyojua ni kwamba marufuku imeondolewa kwa sisi wahudumu wa magari ya uchukuzi wa mizigo.

Bw Elungata alituruhusu kusafirisha mizigo au bidhaa zetu wakati wowote. Inakuaje leo hii tunateswa na wanajeshi? Tunataka ukweli na haki itendeke. Mimi nimeumizwa mkono na hao KDF,” akasema Bw Omar.Kufuatia matukio hayo ya kuteswa kwa madereva na KDF, watumiaji wa barabara ya Lamu-Witu-Garsen, hasa wasafirishaji mizigo wameapa kutosafiri usiku hadi pale watakapohakikishiwa usalama wao barabarani.

“Siwezi kusafirisha mizigo usiku kwa sasa. Lazima serikali iweke wazi iwapo marufuku ya usiku bado ipo au imeondolewa. Tuko na hofu ya kupigwa na hata kuangamizwa na hawa wanajeshi wanaofaa kutulinda sisi raia,” akasema Bw Ahmed Abdallah.

You can share this post!

Mbunge adai roho ya Kingi ingali katika ODM

CHARLES WASONGA: Ushirikiano wahitajika kuzuia ajali msimu...

T L