KDF wavamia kambi ya Al Shabaab msituni Boni, waua wanne

KDF wavamia kambi ya Al Shabaab msituni Boni, waua wanne

MOHAMED AHMED NA KALUME KAZUNGU

KIKOSI maalum cha wanajeshi wa Kenya jana kilivamia kambi ya kundi la magaidi wa Al Shabaab katika msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, na kuwaua wapiganaji wanne na kumkamata mmoja.

Wanajeshi hao waliharibu kambi hiyo kulingana na ripoti za wadokezi wa usalama.Uvamizi huo pia ulipekea kupatikana kwa vilipuzi, maelfu ya risasi pamoja na vifaa vya mawasiliano vilivyoaminika kutumika na magaidi wa kundi hilo haramu ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi wa Lamu.

Gaidi aliyekamatwa anahojiwa na maafisa wa usalamaKulingana na duru katika vitengo vya usalama ambao pia walitutumia picha na video ya operesheni hiyo, kundi la Al Shabaab lilizidiwa wakati wa uvamizi huo wa ghafla katika kambi hiyo msituni.

Baada ya kuwaua magaidi hao, wanajeshi wa Kenya walichoma baadhi ya vitu walivyovipatikana ndani ya kambi hiyo.

Operesheni hiyo imefanyika wiki moja tu baada ya wanachama wa Al Shabaab kujaribu kuvamia gari la maafisa wa polisi waliokuwa wakisindikiza magari ya uchukuzi wa umma eneo la Lamu.

Shambulizi hilo la Jumapili wiki jana lilizimwa na maafisa hao waliokuwa wanasafiri katika barabara ya Lamu-Gamba, eneo la Nyongoro.Tangu kutokea kwa shambulizi hilo, maafisa wa usalama wamekuwa wakiwasaka washukiwa hao wa Al shabaab, ambao waliaminika kutoka Somalia kupitia Garissa hadi Tana River.

Mshirikishi wa Kanda ya Pwani, John Elungata alithibitisha kuwa washukiwa hao wanasakwa na maafisa kufuatia tukio hilo la Nyongoro.

Akizungumza kuhusiana na hali ya usalama wakati wa msimu huu wa likizo, Bw Elungata alisema kuwa usalama umeimarishwa na kuwahakikishia wakazi wasiwe na hofu ya kundi hilo la kigaidi.

‘Vitengo vyetu vyote vimo ngangari kuhakikisha kuwa usalama upo sawa. Juzi mlisikia vile maafisa walipambana na wanamgambo. Hiyo ni kuonyesha kuwa tuko macho na tusiwe na hofu,’ akasema Bw Elungata.

Shambulizi hilo lilijiri siku chache baada ya magaidi kumteka na kumkata kichwa chifu mmoja Kaunti ya Wajir.

You can share this post!

Waislamu waungana kupinga BBI

Wasichana wakeketwa na kuozwa Baringo