Habari Mseto

KEBS kusaka vipodozi hatari vinavyouzwa nchini

January 19th, 2020 2 min read

Na EDWIN OKOTH

SHIRIKA la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS), litaongoza uchunguzi unaojumuisha taasisi mbalimbali kuhusu wafanyabiashara haramu wa kemikali za kugeuza rangi ya ngozi, wanaotengeneza mamilioni kwa kuuza vipodozi vilivyopigwa marufuku na kuhatarisha maisha ya Wakenya wengi.

Wafanyabiashara hao hufanya ulanguzi wa bidhaa hizo kupitia mipaka isiyo na ulinzi mkali na kuziuza Nairobi na miji mingine katika biashara ya mamilioni inayostawishwa na wanawake wenye ngozi nyeusi na wenye kiu cha urembo.

Mbinu mojawapo ya ulanguzi huo ni kuagizia bidhaa hizo nchini na kuzifanya kama zinazosafirishwa Congo lakini zinaachwa nchini huku njia nyingine ikitumia mabasi yanayopitia barabara ya Nairobi-Kinshasa, ambapo bidhaa hizo huingizwa Kenya.

Mkurugenzi wa Kebs, Bw Bernard Njiraini, alieleza ‘Taifa Jumapili’ kwamba kuongezeka kwa vipodozi haramu kumeibua wasiwasi ambao sasa utasababisha msako mkali unaolenga mabwenyenye wanaoagizia nchini vipodozi hivyo vilivyopigwa marufuku.

“Tumepiga marufuku vipodozi kadha ambavyo vinasheheni hydroquinone na mercury na tuna hakika huwa haviingii nchini kupitia vituo halali vya kuingia nchini lakini kupitia mipaka isiyo na ulinzi,”

“Tunabuni mpango utakaojumuisha mashirika mbalimbali pamoja na Idara ya Uchunguzi wa Jinai ili kuwalenga wahusika wakuu na kukomesha kabisa biashara hiyo,” alisema Bw Njiraini.

Kebs tayari ilikuwa imepiga marufuku karibu aina 130 za sabuni na mafuta yanayosheheni aina nane ya kemikali hatari lakini sehemu kubwa ya vipodozi hivyo ingali inasambazwa Nairobi.

Uchunguzi uliofanywa madukani River Road, Duruma na Tom Mboya, ulibainisha kuwa vipodozi hivyo vilivyopigwa marufuku na Kebs kwenye tovuti yao vinauzwa maeneo hayo.

Kebs imesisitiza kwamba bidhaa hizo zinafaa tu kutumiwa kufuatia maagizo ya daktari na kuambatana na muda utakaopendekezwa na daktari.

Bidhaa hizo pia hazipaswi kuuzwa katika soko wazi lakini katika vituo vya kuuzia dawa vilivyosajiliwa.

Bidhaa hizo kando na hydroquinone, zinasheheni kemikali nyinginezo kama vile steroids, mercury na hydrogen peroxide na zinajumuisha sabuni mbalimbali maarufu kama vile Fair Lady, Jambo na Movate.

Miongoni mwa mafuta ya kufanya ngozi kuwa nyeupe yanayosemekana kusheheni mercury na chembechembe zake ni pamoja na Dark & Lovely Cream, Pimplex Medicated Cream, Movate Cream, Skin Success Gel, Peau Claire Cream, Fair & White Gel Plus na mengineyo.

Baadhi ya bidhaa hizo zinazoagizwa kutoka nje zimebadilishwa majina ili kuvutia wateja kama vile Jaribu Cream, Madonna Medicated Cream, Ambi Extra Complexion Cream for Men, Fulani Creme Eclaircissante na Binti Jambo Cream.