Kebs na Inable wazindua kanuni za kuwafaa walemavu kidijitali

Kebs na Inable wazindua kanuni za kuwafaa walemavu kidijitali

Na WANGU KANURI

WAKENYA wanaoishi na ulemavu pamoja na wale  wakongwe sasa wataweza kupokea huduma wanazotaka kidijitali za mawasiliano na habari.

Hii ni baada ya Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) likishirikiana na shirika la inABLE, kuzindua kanuni za kitaifa za mawasiliano na habari zitakazowawezesha walemavu kupata huduma kidijitali.

Uzinduzi huo uliofanyika katika hoteli ya Enshaipai, Naivasha, utawashurutisha wanaotoa huduma za mawasiliano na habari kidijitali, kuhakikisha kuwa huduma hizo zinawafaa walemavu pia.

Baada ya ugonjwa wa covid-19 kuvamia dunia, watu walilazimishwa kutumia jukwaa la kidijitali kufanya mikutano, kusoma na hata kufanya kazi wakiwa nyumbani. Hali hiyo iliwanyima nafasi mamilioni ya watu wakiwemo walemavu.

Bw Wilson Macharia, mshauri anayetetea ujumuisho wa watu wanaoishi na ulemavu na anachora taswira ya jinsi hali ilivyokuwa.

“Kama Mkenya mwenye ulemavu wa kutoona, singeweza kutumia tovuti ya iTax inaomuwezesha mtu kujaza malipo yake ya ushuru. Hii ni kwa sababu kuna swali la hisabati ambalo lazima mtu alijibu ili aweze kuendelea.”

“Mimi kutoweza kulijibu swali hilo kunamaanisha singeweza kujaza malipo yangu ya ushuru jambo ambalo lingevutia penalti kutoka (KRA). Vile vile, singeweza kufika kwenye ofisi za Shirika la Utozaji Ushuru (KRA) ili kupata msaada sababu ya masharti makali yaliyowekwa na Wizara ya Afya ili kudhibiti kuenea kwa Covid-19,” akaeleza.

Hata hivyo, kupitia uzinduzi wa kanuni za kitaifa zitakazowawezesha walemavu kupata huduma za mawasiliano na habari kidijitali, kutakuwepo na kifungu kitakachohitaji kuwepo na mbadala wa sauti au maandishi kwenye tovuti. Hii itawafaa sana watu wenye ulemavu wa kuona.

Mkurugenzi mtendaji wa KEBS Zachary Lukorito, alieleza kuwa uzinduzi wa kanuni hizo utapunguza changamoto ambazo walemavu hupitia wanapopata huduma kwenye jukwaa za kidijitali.

“Kanuni hizi zitasaidia sana katika kuhakikisha kuwa changamoto ambazo walemavu hupitia wakipata huduma zimeshughulikiwa. Kanuni hizi zinawalenga watu wote walio na ulemavu wa kuona, kuongea, kutembea, kufikiria, kusoma na matatizo ya kiakili.”

“Kanuni hizi zitakuwa zimeidhinishwa ifikiapo Aprili 2022 na kuanza kutekelezwa ifikapo mwezi wa Mei 2022,”akaongeza Bw Lukorito.

Mwanzilishi na Mkurgenzi Mkuu katika shirika la inABLE, Irene Mbari-Kirika, kwa upande wake, alisisitiza haja ya walemavu kuwa huru na kuweza kujitegemea.

Hali kadhalika, alieleza kuwa kanuni hizo hazilengi sekta mahususi bali shirika na kampuni zote zinazotumia teknolojia kutoa huduma za mawasiliano na habari kidijitali.

“Ni muhimu kwa wanaounda na kudhibiti sera na wenye biashara kuelewa kuwa wakati tovuti na apu za simu zinatumika kwa urahisi kwa walemavu basi zinawafaa watu wote. Ujumuishaji huu unawapa watu wote nafasi sawa na usiri huku walemavu wakiwa huru,” akaeleza.

Isitoshe, Bi Irene aliwarai wanaounda bidhaa na kutoa huduma kupitia teknolojia kuhakikisha kuwa tovuti au nyenzo wanazotumia, zinanafasi kwa walemavu.

“Wanabiashara wanapaswa kuhakikisha kuwa tovuti watakazotolea huduma au kuuzia bidhaa zao zimewajumuisha watu wote kabla ili kupunguza gharama watakayohitajika kulipa baada ya kanuni hizi kupitishwa na kutekelezwa,”akasema.

Stanley Mutuma, wakili wa mahakama ya juu alieleza kuwa kanuni hizo zitaweza kutekelezwa kortini baada ya kuzinduliwa na kufanywa sheria.

“Kanuni hizi ni ujeo upya na habari njema kwa watu wanaoishi na ulemavu kwani walemavu hawajakuwa wakipata huduma za mawasiliano na habari kidijitali kwa urahisi.

Isitoshe, kupitia kuidhinisha kanuni hizi kama mfumo utakaotumika kisheria, wanaotoa huduma na kuuza bidhaa watapaswa kufuata mahitaji ya kanuni hizi,” akasema.

Hali kadhalika kanuni hizo za kuwashirikisha walemavu kidijitali zitawafaa washika dau wote katika uchumi kama anavyoeleza Bw Bernard Chira, Mkurugenzi wa Innovate Now, Global Disability.

“Kwa kuwa kanuni hizi zinawalenga watu wote, zitawafaa wauzaji na wateja wao. Wenye bidhaa na huduma wataongeza mapato yao kupitia mauzo yao kwa sababu walemavu pia wataweza kupata bidhaa na huduma hizo. Isitoshe, wanaotengeneza programu watapata nafasi za ajira sababu tovuti zote zitapaswa kuwa na nafasi za walemavu kupata huduma.”

Kwa miezi sita ijayo, shirika za inABLE na KEBS zitakuwa zikishirikiana na washikadau wengine wakiwemo; Shirika la Mawasiliano nchini (CA), Baraza la Taifa la Watu Walio na Ulemavu (NCPWD) na Shirika la Masuala ya Mawasiliano na Teknlojia pamoja na wataalam kadha wa kadha katika utunzi wa kanuni hizo.

Kenya kwa sasa ndiyo nchi ya kwanza barani Afrika kuzindua kanuni zitakazowawezesha walemavu kupata huduma za habari na mawasiliano kidijitali.

You can share this post!

Migomo shuleni itafutiwe suluhu

Omanyala atangazwa mwanamichezo bora wa Septemba

F M