Keki anazooka zinapendwa na wateja kote nchini

Keki anazooka zinapendwa na wateja kote nchini

Na MAGDALENE WANJA

BI Catherine Ndung’u amepata umaarufu miongoni mwa wateja wake kutoka sehemu mbalimbali za nchi wanaonunua keki anazooka hasa akiwa mjini Nakuru.

Yeye huoka keki na kuwapelelekea wateja wake katika sehemu mbali mbali nchini.

Bi Ndung’u alisomea kozi ya uandishi wa habari katika chuo kikuu cha United States International University Africa (USIU) ambako alijifunza pia maswala ya uuzaji.

Alipofuzu, alipata kazi katika kampuni ya ujenzi wa barabara jijini Nairobi, kazi ambayo aliifanya kwa muda wa miaka sita.

Safari yake ya kujiajiri ilianza mnamo mwaka 2014 ambapo aliamua kuhamia mjini Nakuru ambako alianza biashara ya kuuza nguo za mitumba.

“Nilijifunza mengi sana kutoka kwa kampuni ile ya ujenzi muhimu zaidi ikiwa ni jinsi ya kufanya biashara,” akasema Bi Ndung’u.

Wakati akifanya kazi ile, alipenda sana kuoka keki wakati wa mapumziko na baadhi ya marafiki wake walipendelea sana kuzila keki alizozioka.

Bi Catherine Ndung’u  akiwa Nakuru. Picha/ Magdalene Wanja

Biashara yake ya kuuza nguo ilimhitaji sana kusafiri na hivyo alikuwa akifika Nairobi mara kwa mara.

“Nilianza kufikiria jinsi ambavyo ningeweza kupata pesa za ziada ambazo zingenisaidia kununua mafuta ya gari ili kupunguza matumizi,” alnasema Bi Ndung’u.

Siku moja alipokuwa akipanga safari yake, aliweka tangazo katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii Facebook akiwauliza marafiki wake jijini Nairobi iwapo wangetaka kununua keki.

La kushangaza ni kwamba alipata idadi kubwa ya watu waliotaka kununua keki zake na akapata faida kubwa.

Mwaka 2016, alianzisha  ukurasa maalum kwa ajili ya kchapisha maelezo kuhusu vyakula mbali mbali pamoja na keki.

Baada ya muda mfupi, aliamua kuianzisha biashara ya upishi ambapo aliandaa chakula katika karamu mbalimbali kama vile harusi, mikutano ya kibiashara, sherehe za kufuzu na za kuzaliwa.

Idadi ya watu ambao walitaka kununua keki jijini Nairobi iliongezeka na hapo ilimbidi kuanza kuifanya biashara hiyo katika sehemu mbali mbali mbali nchini.

Yeye huuza keki moja yenye uzani wa nusu kilo kwa Sh600.

Bi Ndung’u huoka keki kulingana na idadi ya wateja katika sehemu fulani ambao huchukua katika sehemu mbali mbali katika safari yake ambayo humchukua siku nzima.

Katika safari yake ya Nairobi kwa mfano, yeye huuza keki 250, cupcakes dazani 50 na masanduku 40 ya donati yaani doughnuts.

Katika kauti za eneo la Magharibi mwa nchi, yeye huuza idadi sawa na hiyo lakini eneo la Kisii anasema ndilo lenye idadi ya chini zaidi ya wateja.

Bi Ndung’u anasema kuwa kazi hii humpa raha sana haswa anapoona wateja wake wameridhika.

You can share this post!

Barnaba Korir: Tuko tayari kuandaa Kip Keino Classic

Mashabiki wa Schalke washambulia kikosi kwa mayai baada ya...