HabariSiasa

Kelele na Uhuru na Ruto zinavyowatesa wananchi

March 13th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MATUMAINI ya Wakenya kuwa na maisha bora, umoja na usalama yanaendelea kudidimia Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wakiendelea kupambana.

Wachanganuzi wanasema Rais Kenyatta na Dkt Ruto wameweka mbele maslahi na tamaa zao za kibinafsi badala ya maslahi ya raia.

Wabunge, magavana na maseneta wa vyama mbalimbali nao wamefuata nyayo za wawili hao kwa kuegemea upande wa Rais Kenyatta ama wa Dkt Ruto.

Hii imesababisha mijadala ya kusaidia mwananchi wa kawaida kupuuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na kelele za siasa.

Wadadisi wanasema wanasiasa wakiongozwa na rais na naibu wake wameteka nyara nchi na hivyo kutatiza maendeleo pamoja na kuigawanya nchi kisiasa badala ya kuiunganisha wanavyodai.

“Badala ya kuonyesha mfano mwema wa kuigwa na viongozi wengine katika kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakumba Wakenya, rais na naibu wake wanaelekeza nchi pabaya. Hawaaminiani na wamegawa nchi katika mirengo. Huu ndio mwanzo wa masaibu ya Wakenya kwa sababu katika mazingira haya ni vigumu kwa serikali kuhudumia Wakenya kwa njia ifaayo,” aeleza mdadisi wa siasa Tom Maosa.

“Inasikitisha kwamba wanasiasa wanaonekana kutojali matatizo yanayoathiri mwananchi wa kawaida na badala yake wamepagawa na siasa za kubadilisha katiba,” mwanasiasa na mtaalamu wa masuala ya usimamizi Eliud Owalo anafafanua.

“Katika mijadala inayoendelea, anayeumia zaudi ni Mkenya wa kawaida. Wanasiasa hawajali mwananchi. Hata BBI ambayo imetajwa kuwa ya kuunganisha Wakenya imebadilika kuwa ya kuwagawanya zaidi,” asema Bw Maosa.

Aendelea: “Kwa sasa wabunge wanapaswa kuwa wakijadili masuala kama virusi vya corona, gharama ya maisha na nzige. Pia wanafaa kuangazia mbinu za kufanikisha mtaala mpya wa elimu, usalama wa taifa, kufanikisha vita dhidi ya ufisadi na kutafuta suluhu kwa janga la ukosefu wa ajira nchini. Badala yake wanatumia muda wao mwingi kujadili ni nani atakayekuwa rais 2022 na BBI ambayo inagawanya Wakenya zaidi.”

Vita kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto navyo vimeingia baridi huku ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Kupeleleza Uhalifu (DCI) na ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) zikilaumiana.

Lawama za kufifia kwa vita dhidi ya ufisadi imeelekezwa kwa rais na naibu wake kwa kutofautiana kuhusu jinsi ya kuendeleza vita hivyo.

Dkt Ruto amekuwa akikosoa DCI na DPP akisema idara hizo zinatumiwa kumpiga kisiasa huku Rais Kenyatta akitangaza imani yake kamili katika idara hizo.

Bw Owalo anasema vita dhidi ya ufisadi havitafaulu kwani Kenya imetekwa na mitandao ya wafisadi wenye uhusiano na maafisa wa ngazi za juu serikalini.

“Hakuna hatua mathubuti zinazochukuliwa isipokuwa watu kukamatwa Ijumaa na kufikishwa kortini Jumatatu. Kisha wanaachiliwa huru kwa dhamana. Huo ndio unaokuwa mwisho wa vita hivyo,” asema Bw Owalo.

Kulingana na Bw Owalo, suala kuu ambapo wanasiasa kwa sasa wanapaswa kuwa wakijadili ni jinsi ya kupunguza deni la taifa ambalo linaendelea kuongezeka.

“Tumekuwa nchi ya madeni. Hii imesababisha Wakenya kulipa ushuru zaidi. Gharama ya maisha inapanda, hakuna kazi, uchumi unaelekea kukwama na umaskini kuongezeka,” asema.

Kulingana na takwimu, Wakenya zaidi ya 4 milioni hawana kazi, hali inayotokana na viwanda kufungwa kutokana na mazingira mabovu ya kiuchumi na kisiasa nchini.

Ustawi wa viwanda ni moja ya Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee ambazo wadadisi wanasema zitabakia ndoto.

Wiki jana, Ofisi ya Bunge kuhusu Bajeti ilisema hakuna pesa za kufanikisha miradi ya Ajenda Nne Kuu ambazo ni utoshelezaji wa chakula, afya kwa wote, makao nafuu na viwanda.

Mpango wa afya kwa wote nao unakabiliwa na hatari ya kusambaratika kwa kukosa pesa. Ofisi ya Bajeti imesema tangu mpango wa afya kwa wote ulipozinduliwa 2018, hakuna hatua zilizochukuliwa kufanyia mageuzi mashirika yanayohusika ili kufanikisha ajenda hiyo.