Habari

KEMSA: Kagwe sasa atajwa

August 28th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (Kemsa) aliyesimamishwa kazi Jonah Manjari leo Ijumaa amemhusisha Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na sakata ya ufisadi katika mamlaka hiyo.

Akijibu maswali alipofika mbele ya wanachama wa kamati ya seneti kuhusu Covid-19 na ile ya Afya Dkt Manjari amesema kuwa alikiuka sheria wakati wa ununuzi wa vifaa vya kinga (PPE) kutokana na shinikizo kutoka kwa maafisa wakuu wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Bw Kagwe.

Aidha, amesema alipokea maagizo mengine kutoka kwa Katibu katika Wizara ya Afya Susan Mochache ambaye pia ndiye alimshauri kutoa zabuni ya moja kwa moja kinyume cha sheria ya ununuzi wa bidhaa za umma.

“Tuliambiwa tusambaze PPE katika maeneo yaliyoshuhudia visa vingi vya maambukizi ya virusi vya corona kuanzia Machi 2020. Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Katibu Susan Mochache walituamuru kununue vifaa hivyo haraka bila kufuata sheria,” Dkt Manjari akaambia wanachama wa kamati hizo katika ukumbi wa Seneti.

Alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa Bodi ya Kemsa Kembi Gitura.

Maelezo ya Manjari yanakinzana na kauli aliyotoa Bw Kagwe majuzi kwamba hajawahi kuingilia utendakazi wa Kemsa.

“Sikutoa agizo kwa mtu yeyote atoe zabuni. Sijui ni nani alitoa amri kwa Kemsa kuhusu namna ya kutambua kampuni za kuiwasilishia vifaa vya matibabu na dawa,” Bw Kagwe akasema

Dkt Manjari aliwaambia maseneta hivi: “Kando na Kagwe na Bi Mochache, tulipokea maagizo kutoka kwa brigedia fulani ambaye alikuwa akisimamia kamati ya kukabiliana na janga la corona, japo sikumbuki jina lake.”

Afisa huyo aliwaambia maseneta hao, walioongozwa na Seneta wa Trans Nzoia na Seneta Maalum Sylvia Kassanga, kwamba ni kutokana na maagizo hayo ambapo Kemsa ilinunua vifaa hivyo kwa bei ya juu kupita kiasi.

“Kadri idadi ya maambukizi ya corona ilivyokuwa ikipanda ndivyo tuliendelea kuwekewa presha na wakuu wa Wizara ya Afya. Wakati mmoja, walikuja katika maghala ya Kemsa na kutoa maagizo kwamba sharti tusambaze vifaa hivyo, huku wakitisha kutwaa majukumu hayo ikiwa tungejivuta,” Dkt Manjari akaeleza.

Afisa huyo ameelekeza kidole cha lawama kwa wakuu wa Wizara ya Afya siku moja baada ya Bw Gitura kuiambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya kwamba Bi Mochache ndiye aliwapa idhini ya kununua vifaa hivyo kwa bei ya juu.

“Hatufai kulaumiwa kwa kukiuka sheria ya ununuzi na hivyo kusababisha hasara ya mabilioni ya fedha kwa sababu tulikuwa tukipokea amri kutka kwa Katibu wa Wizara Bi Mochache,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Bi Sabina Chege.

Bw Gitura aliiambia kamati hii kwamba Katibu huyo wa Wizara ndiye aliamua vifaa vya kununuliwa, mahala pa kununua na bei, hatua ambayo alisema ni kinyume cha sheria kwa sababu halmashauri hiyo haifai kuelekezwa wizara hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kemsa inalaumiwa, kwa mfano, kwa kununua barakoa aina ya N95 (1860) kwa Sh1,300 kila moja badala ya bei ya kawaida ya Sh700.

Wabunge walielezwa kuwa wakati huu halmashauri hiyo ingali inashikilia PPE za thamani ya Sh6.2 bilioni ilizonunua kwa bei ghali na ambazo sasa imeshindwa kuuza kwa sababu bei ya vifaa hivyo imeshuka.