Habari za Kitaifa

Kemsa yampiga kalamu kaimu mkurugenzi wa ununuzi

February 21st, 2024 2 min read

STEVE OTIENO Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA Usambazaji Vifaa vya Matibabu Nchini (Kemsa) imemsimamisha kazi kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi Gilbert Mamati kwa ukiukaji wa sheria za ununuzi na kufanya mabadiliko ya wafanyakazi katika idara hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa wiki mbili baada ya bodi ya Kemsa kupokea ripoti ya ukaguzi wa ndani kuhusu zabuni zilizotolewa kati ya Julai na Desemba 2023.

Ukaguzi huo ulilenga kuhakikisha uwepo wa uwazi katika shughuli za ununuzi katika mamlaka hiyo.

Akiwahutubia wanahabari katika kituo cha usambazaji bidhaa za Kemsa eneo la Embakasi Jumatano, Mwenyekiti wa bodi hiyo Irungu Nyakera alisema uwazi na uwajibikaji ni nguzo kuu zitakazotumiwa kufanikisha mabadiliko katika Kemsa.

“Ukaguzi ulioendeshwa ulichanganua zabuni za thamani ya Sh5 bilioni na kutambua dosari kadha. Ni ni pamoja na utoaji kwa kampuni ambazo hazikufaulu kutimiza vigezo vya kisheria. Ilibainika kuwa baadhi ya kampuni hazikuwa na uwezo wa kiteknolojia wa kutekeleza matakwa ya zabuni hizo,” akasema Bw Nyakera.

“Kwa hivyo, tumefanya mabadiliko katika uongozi wa Idara ya Ununuzi bidhaa na kuwatuma maafisa wa hazina ya kitaifa kuisimamia na kufanya mabadiliko mengine ya wafanyakazi. Aidha, tumeanzisha mchakato wa uteuzi wa mkurugenzi mpya wa idara ya ununuzi,” Bw Nyakera akaongeza.

Ndani ya miaka minne iliyopita Kemsa haijakuwa na mkurugenzi wa kudumu wa Idara ya Ununuzi baada ya kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa mshikilizi wa wadhifa huo Charles Juma mnamo 2020 kutokana na sakata ya ununuzi wa bidhaa za kupambana na Covid-19 za thamani ya Sh7.6 bilioni.

Bw Nyakera alisema bodi hiyo imejitolea kulainisha shughuli za Kemsa ili kuimarisha utoaji huduma na hivyo kuwaridhisha wateja.

“Hii itarejesha imani ya umma na wateja kwa Kemsa, kuondoa ufisadi, kuimarisha uongozi, kuongeza faidi, kuwapa motisha wafanyakazi ili waimarisha uzalishaji,” akaeleza.

Ili kuzuia visa vya kutokea kwa dosari katika ununuzi siku zijazo, Nyakera akaongeza, Kemsa inaendesha ukaguzi wa wafanyakazi katika idara ya ununuzi kubaini viwango vyao vya maadili. Mageuzi hayo pia yatazuia hali ambapo mfanyakazi anahudumu katika kituo kimoja kwa muda mrefu.

“Aidha, bodi imezima mwenendo wa utoaji wa zabuni ya moja kwa moja kwani hii inatoa mwanya wa ufisadi.

“Kwa hivyo, zabuni zote zitakaguliwa kwa kina na usawa na zile ambazo hazijatimiza viwango hitajika vya kisheria zitatemwa. Ukiritimba katika utoaji zabuni umezimwa kabisa,” akasema Bw Nyakera.

Mwenyekiti huyo wa Kemsa pia aliahidi kuwa ifikapo mwishoni mwa Machi 2024, uwekaji wa mfumo wa ununuzi kimtandaoni (e-procurement) utakuwa umekamilishwa.

“Kwa kukumbatia mfumo huo, tunalenga kulainisha shughuli za ununuzi bidhaa na utoaji zabuni katika Kemsa na kuzifanya kuwa wazi na zinazoimarisha uwajibikaji. Kupitia njia hii tutazima kabisa katika uozo wa ufisadi haswa katika idara hii ya ununuzi,” akaeleza.