KEMSA yatangaza zabuni nyingine ya bidhaa za corona sakata ya 2020 ikisalia kitendawili

KEMSA yatangaza zabuni nyingine ya bidhaa za corona sakata ya 2020 ikisalia kitendawili

NA EDWIN MUTAI 

MAMLAKA ya Usambazaji wa Dawa Nchini (Kemsa) inapanga kununua bidhaa zaidi za kupambana na Covid-19 licha ya kutotanzuliwa kwa sakata ya kupotea kwa Sh7.8 bilioni kupitia ununuzi wa bidhaa hizo kwa bei ya juu kupita kiasi.

Mamlaka hiyo, inayofanyiwa mageuzi, kutokana na changamoto za kifedha na kiusimamizi, imewataka wafanyabiashara kutuma maombi ya zabuni ya kuiuzia bidhaa za Covid-19.

“Kwa niaba ya serikali na Wizara ya Afya, Kemsa inatangaza zabuni ya ununuzi wa bidhaa za Covid-19, awamu ya tatu,” Kemsa ikaseMa kwenye notisi iliyotoa Ijumaa.

Kulingana na notisi hiyo iliyochapishwa katika magazetini, kampuni husika zinatakiwa kuwasilisha maombi yao kabla au mnamo Februari 10, 2022.

Kemsa inatoa zabuni hiyo chini ya kitengo cha shirika la Global Fund kuhusu uwasilishaji wa bidhaa za Covid-19.

Kemsa pia ilitangaza zabuni tofauti ya ununuzi wa mitungi ya hewa ya oksijeni na oksijeni ya majimaji inayotumiwa kuwatibu wagonjwa chini ya ufadhili wa shirika la AFD.

Zabuni mpya ya ununuzi wa bidhaa za Covid-19 iliyotolewa na Kemsa huenda ikaibua hisia kutoka kwa Wakenya kufuatia sakata ya ununuzi wa bidhaa hizo mnamo Machi 2020 kwa bei ya juu kupita kiasi.

Kemsa ilinunua bidhaa hizo kwa Sh6.3 bilioni katika ununuzi ambao Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iligundua kuwa ilitolewa kinyume cha sheria.

Sakata hiyo pia ilichunguzwa na kamati za bunge la kitaifa na seneti ambazo zilibaini kuwa bidhaa hizo zilinunuliwa kwa bei ya juu kupita kiasi.

Chunguzi hizo zilielekeza kidolewa cha lawama kwa maafisa wakuu wa Kemsa wakiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Jonah Manjari ndio walihusika katika uovu huo.

Katika ripoti zao, EACC na kamati za bunge zilipendekeza kwamba Bw Manjari na wakurugenzi; Eliud Muriithi (Idara ya Biashara)  na Charles Juma (Idara ya Ununuzi) wafunguliwe mashtaka.

Baadaye, maafisa hao walisimamishwa kazi na bodi ya usimamizi wa Kemsa.

Kando na hayo, ukaguzi maalum ulioendeshwa na afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathangu ulionyesha kuwa huenda Kemsa ikapoteza Sh2.33 bilioni ikiwa bidhaa  za kukinga corona zilizoko katika maghala ya mamlaka hiyo kote nchini zitauzwa kwa bei ya sasa.

Ukaguzi huo ulionyesha kuwa Bw Manjari alikataa bei ya chini ilitolewa na baadhi ya kampuni zilizotaka kuuzia Kemsa bidhaa za kupambana na Covid-19 kwa bei nafuu.

Kulingana na ripoti ya ukaguzi huo maafisa wa Kemsa waliamua kununua paketi moja yenye barakoa 50 kwa Sh4,500 badala ya bei kawaida ya Sh3,183.

Paketi moja ya tembe za kupunguza maumizi, Paracetamol, ambazo hununuliwa kwa Sh40 zilinunuliwa kwa Sh66.50 huku sanitaiza ambayo huuzwa kwa Sh313 ilinunuliwa kwa Sh494, kulingana na ripoti hiyo.

Kulingana mkaguzi huyo wa hesabu za serikali kando na kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu kupita kiasi, Kemsa ilikosa kufanya uchunguzi kuhusu mahitaji ya bidhaa hitaji za corona.

Kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC) katika ripoti yake ilipendekeza kuwa kampuni 110 zilizouzia Kemsa bidhaa hizo kwa bei ya juu kupita kiasi zirejeshe pesa za ziada zilizolipwa.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir pia ilipendekeza kuwa shirika la kutwaa mali ya wizi (Assets Recovery Agency-ARA) itwae mali kama vile magari, nyumba na ardhi, zilizonunuliwa kwa kutumia pesa zilizopatika kupitia sakata ya Kemsa.

Aidha, PIC inamtaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), James Gathii Mburu, kuanzisha uchunguzi dhidi ya kampuni zote zilizouzia Kemsa bidhaa za Covid-19 kubaini ikiwa zililipa ushuru.

Lakini licha ya chunguzi kadha kupendekeza kushtakiwa kwa Bw Manjari na wenzake, afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji imedinda kufanya hivyo. Bw Haji anasema afisi yake ingali inakusanya ushahidi kwa kuhimili kesi hiyo.

TAFSIRI: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Nation FC yazima Dagoretti Hot Stars na kutwaa ubingwa wa...

Ripoti yaanika jinsi makocha hutekeleza dhuluma za kimapenzi

T L