Kendia FC ya Ruiru yapiga hatua

Kendia FC ya Ruiru yapiga hatua

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya Kendia FC ya Ruiru ni timu ambayo imefanikiwa kupiga hatua ya haraka kwa kipindi cha muda mfupi tangu ibuniwe.

Kocha Moses Nyawanga, anasema alibuni klabu hiyo mwaka wa 2020 na mwaka uliofuata wa 2021 alisajili timu hiyo kucheza ligi ya kaunti ndogo ya Ruiru.

Tayari anajivunia kuibuka kama bingwa wa ligi ya kaunti ndogo ya Ruiru, iliyojumuisha timu 20.

Timu ya Kendia ilijikakamua na kuibuka bingwa wa ligi hiyo na pointi 76.

Hivi sasa timu hiyo inashiriki katika ligi ya kaunti ya Kiambu.

Kikosi chake ni cha wachezaji 24.

Timu hiyo iko chini ya ufadhili wa kampuni ya kuunda magunia ya nailoni ya Kendia iliyoko mjini Ruiru.

Hata hivyo, timu hiyo inajisimamia kwa maswala mengine kadha licha ya kufadhiliwa na kampuni hiyo.

Kocha Nyawanga anakiri ya kwamba pia amefanya mengi kwa wachezaji wake kwa sababu amehakikisha kila mchezaji anapata ajira katika kampuni hiyo.

“Nilihakikisha kila mchezaji amepata ajira ili kila mmoja awe na ari ya kutandaza soka bila wasiwasi wowote,” alifafanua kocha huyo.

Alisema kwa mara ya kwanza kampuni ilinunua vifaa muhimu vya michezo kama viatu, jezi na mipira.

Anasema msimu huu ameweka mikakati itakayofanya timu hiyo kupiga hatua zaidi ili kupanda katika kiwango kingine.

“Mimi kama kocha nilifanya juhudi kuwaleta pamoja vijana mitaani na kuunda timu moja itakayowapa mwongozo wa kimaisha. Nataka kubadilisha tabia ya vijana kabisa hapa mjini Ruiru,” akasema alipohojiwa na safu hii.

Kocha analenga kunoa vijana hao ili wawe wanasoka wa kutegemewa katika siku zijazo.

Wanasoka wanaoipa uhai klabu hii ni Evans Juma (kipa), madifenda ni Zadock Chonge, Isaac Wanjala, Victor Wabakawa, na George Wasije.

Kiungo cha kati kuna Bramwel Masinde, John Walekhwa, na Kevin Situma. Mastraika ni Riziki Muemah, na John Wanjala.

Kocha huyo aliwahi kuchezea timu ya Matopeni eneo la Komorock jijini Nairobi.

Kulingana na kocha huyo anasema msimu huu atazingatia nidhamu miongoni mwa vijana wake huku mazoezi ya kila mara pia yakitiliwa maanani.

Bado anatoa wito kwa wahisani popote walipo wajitokeze kwa hali na mali ili kuwapa ufadhili wowote ule kwa sababu ligi ya kaunti ya Kiambu inahitaji usafiri wa kila mara.

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili cha Triple ‘S’ katika shule...

Githua: Gaspo tunahitaji taji la ligi kuu msimu huu

T L