KENNEDY OSORE: Soka inavyokuza maadili katika jamii

KENNEDY OSORE: Soka inavyokuza maadili katika jamii

NA PATRICK KILAVUKA

Ni vyema mja kupanda mbegu ambayo itazaa kwa vizazi hadi vizazi. Huo ni ushauri na ushawishi uliomsukuma kocha Kennedy Osore wa timu ya Lopez FC, Kangemi kuibuni timu hii kama njia ya kutimiza ndoto ya talanta yake baada ya kupata jeraha ambalo lilimsaza goti na kumwezesha kuangika buti zake kwa mujibu wa ushauri wa daktari baada ya upasuaji uliofualu akiwa kinda.

Mkufunzi Osore alianzisha timu hii na wachezaji waliokuwa na umri wa miaka chini saba mwaka wa 2009 baada ya kupona na timu imedumu kwa miaka kumi na moja huku wengi wa wanasoka waanzilishi wakiwa ndoano ya kuvuta wengine baada ya timu kunawiri na hata kushiriki vipute na ligi za hadhi za Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Anadokeza kuna wachezaji zaidi ya mia hamsini ambao wamepitia mikononi mwake na wanasakatia timu za mitaani na ligi.

Kikosi cha Lopez kiko chini ya meza ya kiufundi ya kocha huyo, timu meneja Jacob Onyari na nahodha John Wamera na kinafanyia mazoezi uga wa Kihumbuini.

Kimeweza kupambana na changamoto mbalimbali kama ukosefu wa kifedha kugharamia timu ligini, vifaa vya michezo na kadhalika japo timu inajipa moyo konde kuona kwamba, inafikia ufanisi wa kucheza ligi za daraja ya juu.

Kwa kiasi kanisa la ACK St Paul, Waruku linaihisani pamoja na wachezaji kulisha kiroho na kukuzwa imani kwani, baadhi ya wanasoka hao ni wafuasi.

Picha hii iliyoipigwa miaka 9 iliyopita inamwonyesha Kennedy Osore kwenye timu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 9 Kangemi. PICHA/ PATRICK KILAVUKA

“Kanisa limetusaidia na msaada wa kiroho mbali na kuwasaidia baadhi ya wanasoka kupata mafunzo ya taaluma ya tarakilishi, stima na kuelimisha wengine kuwa wahamasishaji wa vijana kuhusu majanga ya magonjwa kupitia mpango wa UNICEF.

“Na, hali hiyo ya uhamasisho imeleta mtazamo chanya miongoni mwa jamii na kuboresha maadili mema, ” asema kocha Osore aliyehitimu cheti cha ukocha wa kiwango cha CAF C kilichoidhinishwa baada ya kupata mafunzo mwaka 2019 ambayo yalifanyika katika Taasisi ya Goan.

Matumaini yenye mazao ya kocha huyo yaliiwezesha timu kujituma katika ligi tangu mwaka wa 2015 iliposhiriki Ligi ya Kauntindogo ya Shirikisho la Soka Nchini na kutwaa namba tatu hali sawa na mwaka 2016 ilipopandishwa ngazi kushiriki Ligi ya FKF, Kaunti, tawi la Nairobi Magharibi (NWCL) na kuonesha makali yake kisha kuinuliwa kucheza Ligi ya Kanda ya Nairobi Magharibi (NWRL) ya Shirikisho hilo ambapo ilimaliza ya Kumi na sita mwaka 2017 na hivyo basi kujikwaa na kuingia katika ulazima wa kujitosa katika Ligi ya Kaunti ya tawi la Nairobi Magharibi, mwaka 2018 na kuihitimisha katika nafasi ya saba bora.

Timu inayonolewa na kocha Osore mwaka wa 2018. PICHA/ PATRICK KILAVUKA

Aidha, mwaka 2019 ilicheza kiwango cha hicho cha Kaunti japo msimu huo ulisitishwa kutokana na msambao wa ndwele ya corona. Ilikuwa imecheza michuano mitatu dhidi ya Gachie Soccer na kuibwaga 1-0 kabla kuandikisha sare mbili za 2-2 mbele ya Cheza Sports na UoN Olympic mtawalia.

Fauka ya hayo, wanayomatumaini ya kupanda ngazi katika Ligi ya Kanda ya FKF, tawi la Nairobi Magharibi (NWRL) kwa mara nyingine tena ila, wanaogojea idhinisho la Shirikisho hilo kurejelewa kwa ligi.

Fito za timu ambazo zimewahiwa kujenga vikosi vya hadhi katika ulimwengu wa dimba na ambavyo vimepitia mikononi mwa kocha huyo ni Allan Mwala aliyekambini Nairobi Stima, Christopher Ambulance ( Kangemi Allstars), Sammy mwita( Bandari Youth), Oliver Owour (Chemilili), Jossiah Simiyu (U-20 Harambe Stars) na George Wamere (Gor Mahia Youth).

Timu yake ikijiandaa kwa mechi mtaani Kangemi 2020. Picha/ PATRICK KILAVUKA

Kando na kushiriki ligi, timu hii imeshirika makala yote saba ya kipute cha Tim Wanyonyi Super Cup na mwaka huu ilifika nusu fainali ya king’ang’anyiro hicho japo ilibanduliwa na Young City 2-0.

Mipango ambayo ipo hai kwa timu ni kushiriki Ligi ya Kanda, kukuza zaidi vipawa vya soka na kusaka ufadhili.

Kikosi kamili ni Richard Mukirai, Steve Oumwa, Fanthew Ashiona, Caleb Ombuna, Sabestian Shavola, Ephraim Kanaki, Benard Omungala, Biden Ndwiga, Kevin Kaunda, George Kuria, Eutichus Simiyu, Mark Chokora, John Namae, Chrispus Wambua, Hillary Evisa, George Mbugua na George Wamera

You can share this post!

Trump kwisha!

South C Ladies: Soko inavyowasisimua mabinti wa mitaani