Habari Mseto

Kenya Airways kushirikiana na Alitalia

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya ndege ya Kenya Airways imeingia katika mkataba na kampuni kubwa zaidi ya ndege ya Italia, Alitalia, kwa lengo la kuimarisha huduma zake.

Kampuni hizo zinalenga kuwapa wateja wake chaguo zaidi la ndege ambazo wanatumia kati ya Nairobi na Rome.

Mkataba huo ulianza kutekelezwa Alhamisi ambapo huduma za ndege za Alitalia zitaendelezwa na kutangazwa na ndege za Kenya zaidi ya ziara za Nairobi, Mombasa na Kisumu lakini katika miji 19 ambako ndege za Kenya Airways huzuru ikiwemo ni pamoja na Abidjan, Accra, Addis Ababa, Antananarivo, Brazzaville, Dar es Salaam na Douala.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha ziara kwa kuwapa wateja ziara za moja kwa moja kutoka Rome.

Hali itakuwa kama hiyo kwa Kenya Airways ambapo huduma zake zitapanuliwa kwa kutangazwa na Alitalia Rome na Ulaya katika miji 16, ilisema KQ katika taarifa.

Kampuni ya Alitalia na Kenya Airways ni kati ya kampuni za ndege ambazo ni wanachama wa SkyTeam Alliance.

Kenya Airways itazindua ziara za kila wiki kati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Uwanja wa Kimataifa wa Leonardo da Vinci, Fiumicino, Rome, Juni 12, 2019.

Alitalia hufanya ziara katika miji 77 ikiwemo miji 22 ya Italia na 55 ya kimataifa ambapo hufanya ziara kufikia 3,600 kwa kutumia njia 102.