Habari Mseto

Kenya Airways yaanzisha safari za kila siku Somalia

November 14th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Uchukuzi wa Ndege, Kenya Airways limethibitisha kuwa limeanzisha safari za kila siku za moja kwa moja kati ya Nairobi na Mogadishu.

Kutakuwa na ziara moja kurejea nchini kutoka Somalia kila siku, ilisema KQ.

Ziara hizo zitaanza Alhamisi. Kulingana na KQ, safari hizo zilianzishwa kutokana na ongezeko la mahitaji katika njia hiyo na hatua hiyo inatarajiwa kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili.

“Hatua ya kuongeza safari hiyo inaonyesha kujitoa kwetu katika kuimarisha uchukuzi barani Afrika pamoja na kuunda nafasi kwa mashirika, wawekezaji, wafanyibiashara na watalii,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa KQ Sebastian Mikosz katika taarifa.

Ndege hiyo itakuwa ikiendeshwa na Jambojet, Bombardier Dash 8 Q400,na itakuwa ikiondoka JKIA kila siku saa mbili kasoro dakika 20 kila siku na kuondoka Uwanja wa Kimataifa wa Aden Adde Mogadishu saa tano kasorobo asubuhi ili kuwasili Nairobi saa saba mchana.

Huenda KQ inashindana na Ethiopia Airlines iliyoanzisha tena ziara zake Aden Adde Novemba 2, baada ya karibu nusu karne, kutoka miaka ya 1970 ilipobatilisha ziara hizo kutokana na mgogoro kati ya mataifa hayo.