Kenya Airways yatangaza hasara kubwa ya Sh36.6b

Kenya Airways yatangaza hasara kubwa ya Sh36.6b

Na PETER MBURU

SHIRIKA la Ndege la Kenya Airways (KQ) Jumanne lilitangaza kupata hasara ya Sh36.6 bilioni mwaka uliomalizika, ambacho ni kiwango cha juu zaidi katika miaka mitano iliyopita.

Kiasi hicho pia ni mara tatu zaidi ya hasara lililopata mnamo 2019. Mwaka huo, shirika hilo lilipata hasara ya Sh12.9 bilioni.

Tangu 2016, shirika hilo limekuwa likipata hasara ya zaidi ya Sh 6 bilioni kila mwaka.

Janga la corona lilichangia kuvuruga mwelekeo wake, kwa kuwa hasara yake iliongezeka kwa zaidi ya Sh20 bilioni.

Ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kupitisha hasara yake Sh30 bilioni.

Mnamo 2017, KQ ilipata hasara ya Sh6.3 bilioni, 2018 Sh7.5 bilioni huku kiwango hicho kikiongezeka na kufikia Sh12.9 bilioni mnamo 2019.

Mnamo 2016, shirika hilo lilipata hasara ya Sh10.2 bilioni. Mapato yake pia yalipungua hadi Sh52.8 bilioni mwaka uliopita kutoka Sh128.9 bilioni mnamo 2019.

Usimamizi wake ulitaja hali hiyo kuchangiwa na janga la virusi vya corona. Mapato kutoka kwa abiria yalipungua kwa Sh69.9 bilioni.

“Sababu kuu ya matokeo hayo ni kupungua kwa idadi ya abiria, hasa kati ya Julai na Septemba. Wakati huo ndio huwa tunarekodi idadi kubwa zaidi ya wateja. Hata baada ya safari za ndege kurejelewa upya Agosti, idadi ya abiria ilikuwa ya chini mno. Licha ya hali kuanza kuimarika Novemba na Desemba, muda huo haukutosha kurejesha mapato tuliyokuwa tumepoteza,” akasema Msimamizi Mkuu wa Masuala ya Fedha katika shirika hilo, Bi Hellen Mwariri.

Shirika pia lilisema hasara hiyo ilichangiwa na Sh7 bilioni zilizotokana na baadhi ya ndege kuharibika.

Licha ya matokeo hayo, liliokoa kiwango kikubwa cha fedha za matumizi kwa kuwa ndege nyingi hazikuwa zikiwabeba abiria.

Kijumla, kiwango cha matumizi yake kilishuka kutoka Sh141.2 bilioni hadi Sh89.3 bilioni.

You can share this post!

Raila, Uhuru waamua kupimana nguvu Kisii

TAHARIRI: Covid: Matumizi ya pesa yaanikwe