Habari za Kitaifa

Kenya bado yalengwa na magaidi – ripoti

March 20th, 2024 2 min read

NA STEVE OTIENO

KENYA ni miongoni mwa nchi 20 zinazoongoza kwa kushambuliwa na magaidi katika orodha inayotawaliwa na mataifa ya Afrika isipokuwa Syria, Pakistan, Israel, Iraq, Chile na Ufilipino.

Hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya hivi punde ya Global Terrorism Index, 2024, ambayo inaonyesha kuwa jumla ya vifo 8,532 vilitokana na ugaidi mwaka 2023, takwimu zinazoonyesha ongezeko kubwa la asilimia 15 kutoka mwaka uliotangulia.

Kwa wastani wa alama 5.6 kati ya 10, huku 10 zikiwa mbaya zaidi, Kenya ilishuka nafasi moja kutoka 17 hadi 18 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti huo wa 2023.

Jambo la kufurahisha ni kwamba, licha ya kushuka kwa viwango, ripoti ilionyesha kuwa hatari ya Kenya kuhusiana na ugaidi ilishuka kutoka kiwango cha ‘juu sana’ hadi ‘kati’, kuonyesha nchi imeboresha mifumo yake ya kupunguza athari za itikadi kali.

Kuimarika huku ni dhihirisho la ushirikiano wa mashirika mbalimbali ya usalama nchini dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shaabab ambalo limeendelea kufanya mashambulio Lamu na maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi.

Katika mwaka uliopita, kuharibiwa kwa kambi kadhaa za muda na kukamatwa kwa wanachama wa kundi hilo na vikosi vya usalama vya Kenya pia kumefanya vigumu kwa kundi haramu kuhudumu kwa urahisi.

Lakini hii haikuja bila gharama. Mnamo 2023, Kenya ilishuhudia mauaji ya kushangaza zaidi katika maeneo ya Lamu, Garissa, Wajir na Mandera.

Mwezi Juni pekee, takriban watu 20 waliuawa katika mashambulio mabaya yaliyotekelezwa na Al-Shabab. Katika shambulio moja la aina hiyo, watu watano walikatwa vichwa na nyumba kuchomwa moto katika vijiji vya Salama na Juhudi katika tarafa ya Mkunumbi, Kaunti ya Lamu.

Huu ulikuwa mwaka wa tisa mfululizo kwa kundi hili kuhusika na vifo zaidi ya 400 kutokana na ugaidi na zaidi ya mashambulio 100 kwa mwaka husika, ripoti ilionyesha. Mnamo 2023, kundi hilo lilihusika na vifo vya watu 26 huko Lamu na wengine 37 katika kaunti za Garissa na Mandera.

Utafiti huo pia uligundua kuwa Al-shaabab linazidi kuimarika, huku asilimia 41 ya mashambulio yake mwaka 2023 yakilenga wanajeshi, wakifuatiwa na raia kwa asilimia 22.

“Al-shaabab ilihusika na vifo 70 nchini Kenya mwaka wa 2023, idadi kubwa zaidi tangu 2019. Operesheni za kukabiliana na ugaidi zinazoongozwa na serikali nchini Somalia zimesababisha kuongezeka kwa wapiganaji wa Al-shaabab wanaovuka mpaka kuingia Kenya, hali inayosababishwa na uhaha wa maafisa wa usalama mpakani,” ilisema ripoti hiyo.

Somalia inayopakana na Kenya ni nchi ya pili hatari kwa ugaidi barani Afrika, ikiwa na alama 7.8. Ulimwenguni, inashika nafasi ya saba na inasalia kuwa nchi hatari zaidi kwa ugaidi.