Michezo

Kenya Cup haitakuwa mchezo msimu ujao – Chenge

December 13th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MCHEZAJI wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya, Davis Chenge amebashiri kuwa Ligi Kuu (Kenya Cup) ya msimu ujao itashuhudia ushindani mkali.

Klabu yake ya KCB imetawala ligi hiyo ya klabu 12 miaka ya hivi karibuni ikishinda mwaka 2015, 2017, 2018 na 2019 na ilikuwa imetinga nusu-fainali ya mwaka 2020 ambao ulivurugwa kabisa na janga la virusi vya corona tangu mwezi Machi.

Sababu kubwa aliyotoa mchezaji huyo wa zamani wa Western Bulls katika utabiri wake ni jinsi klabu zilizoimarisha vikosi vyao sokoni katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichokamilika majuma mawili yaliyopita.

Pamoja na mabingwa wa mwaka 2016 Kabras Sugar, ambao walimaliza juu ya jedwali katika msimu wa kawaida wa 2019-2020, KCB wamekuwa katika orodha ya timu zinazopigiwa upatu kuwa wagombea halisi wa taji kwa misimu kadhaa sasa.

Hata hivyo, Chenge anasema, “Sioni timu ambayo unaweza kusema iko juu kuliko nyingine wakati huu. Nasema hivyo kwa sababu klabu zimenunua na kuuza wachezaji. Nyingine zimeajiri wakufunzi wapya kwa hivyo ni mapema sana kuanza kusema kuna timu nzuri zaidi.”

Chenge, ambaye ameajiriwa na benki ya KCB katika idara ya masuala ya teknolojia, aliongeza, “Ligi itakuwa mpya kabisa. Itakapoanza halafu tuone mechi kadhaa, itatupa picha nzuri nani anaweza kutoa ushindani hadi kipenga cha mwisho.”

Mabingwa mara saba KCB walikuwa katika orodha ya timu zilizokuwa na shughuli chache sokoni baada ya kusaini Wilfred Waswa Mark pekee kutoka Northern Suburbs.

Mabingwa wa zamani Kenya Harlequin, ambao walifanya vibaya sana msimu uliopita, walitikisa sokoni walipotangaza kuajiri wachezaji saba wakiwemo mastaa Joshua Chisanga, Emmanuel Mavala na Philip Ikambili kutoka Homeboyz. Quins pia wameajiri kocha wa kigeni Antoine Plasman kutoka Ubelgiji na huenda wakahangaisha msimu ujao. Serikali bado haijaidhinisha kurejea kwa raga viwanjani kwa hivyo haijulikani msimu utaanza lini, ingawa Shirikisho la Raga Kenya (KRU) limependekeza Januari 2021.