Michezo

KENYA CUP: Kabras Sugar kukabili mabingwa watetezi KCB

November 29th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

VIONGOZI Kabras Sugar watafukuzia muujiza wa kushinda mabingwa watetezi KCB kwa mara ya kwanza watakapomenyana  Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) ya raundi ya sita.

Wanabenki wa KCB, ambao wataalika Kabras kutoka kaunti ya Kakamega uwanjani Ruaraka, hawajawahi kupoteza dhidi ya wanasukari hao katika mechi 10 mfululizo za ligi tangu Kabras ipandishwe daraja mwaka 2014.

Kabras ya kocha Henley Du Plessis imepoteza mechi tisa dhidi ya KCB na kutoka sare mara moja ligini. Vijana wa Du Plessis wamekuwa akifanya vizuri ligini tangu mwaka wao wa kwanza 2014. Hata hivyo, bado wanatafuta ushindi wao wa kwanza kabisa dhidi ya KCB.

Makocha Curtis Olago (KCB) na Du Plessis wameshataja vikosi watakavyotumia katika mchuano huo muhimu, ambao klabu zote mbili zinaweka hatarini rekodi zao za kutoshindwa msimu huu.

Baadhi ya wachezaji Olago anatumai kutumia kuendeleza rekodi nzuri dhidi ya Kabras ni nahodha Curtis Lilako, Oliver Mang’eni, Davis Chenge, Martin Owilah, Shaban Ahmed na Samuel Asati.

Naye, Du Plessis anajivunia wachezaji wakali kama Lawrence Buyachi, George Nyambua, Brian Tanga, raia wa Fiji Jone Kubu na Avisai Kuruyawa na Mganda Asuman Mugerwa.

Takwimu za ana kwa ana kati ya KCB na Kabras Sugar:

Novemba 8, 2014 – KCB 13 Kabras Sugar 3 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Machi 14, 2015 – KCB 27 Kabras Sugar 3 (fainali ya ligi, RFUEA)

Desemba 19, 2015 – KCB 40 Kabras Sugar 15 (msimu wa kawaida wa ligi, Railway Club Nairobi)

Juni 18, 2016 – KCB 24-12 Kabras Sugar (fainali ya Enterprise Cup)

Desemba 3, 2016 – Kabras Sugar 15 KCB 15 (msimu wa kawaida wa ligi, Kakamega)

Januari 28, 2017 – KCB 22 Kabras Sugar 17 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Aprili 22, 2017 – KCB 36 Kabras Sugar 8 (fainali ya ligi, Ruaraka)

Februari 24, 2018 – KCB 41 Kabras Sugar 12 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Machi 24, 2018 – KCB 29 Kabras Sugar 24 (fainali ya ligi, Ruaraka)

Februari 23, 2019 – KCB 44 Kabras Sugar 20 (msimu wa kawaida wa ligi, Impala)

Mei 18, 2019 – Kabras Sugar 15 KCB 23 (fainali ya ligi, Kakamega)

Ratiba ya Novemba 29 (mechi zote zitaanza saa kumi jioni): KCB na Kabras Sugar (Ruaraka), Kenya Harlequin na Mwamba (RFUEA), Nakuru na Impala Saracens (Nakuru Athletic), Menengai Oilers na Nondies (Moi Showground, Nakuru), Homeboyz na Blak Blad (Jamhuri Park), Western Bulls na Kisumu (Kakamega)