Michezo

KENYA CUP: KCB yadunga Kabras Sugar mwiba mchungu katika fainali

May 18th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Jacob Ojee ameongoza KCB kushinda Ligi Kuu ya Raga nchini almaarufu Kenya Cup baada ya kuifungia alama 18 ikirarua Kabras Sugar 23-15 katika fainali uwanjani Kakamega Showground, Jumamosi.

Ojee, ambaye ni nahodha wa timu ya Shujaa itakayokuwa nchini Uingereza kwa duru ya tisa ya Raga ya Dunia mnamo Mei 25-26, aliweka KCB kifua mbele 7-0 alipopachika mguso na mkwaju. Mabingwa wa Kenya Cup mwaka 2016, Kabras walipunguza mwanya huo hadi alama mbili kabla tu ya mapumziko kupitia kwa mchezaji mwingine wa Shujaa, Daniel Sikuta.

Kabras kisha ilichukua uongozi 15-7 baada ya kufunga mguso kutoka kwa Charlton Mokua na mkwajua na penalti kutoka kwa Mganda Philip Wokorach mapema katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, juhudi za Kabras kulipiza kisasi zilizimwa pale Shaban Ahmed alifunga mguso uliondamana na mkwaju kutoka kwa Ojee, ambaye pia aligonga msumari wa mwisho kupitia penalti.

KCB ya kocha Curtis Olago sasa inajivunia mataji ya ligi ya mwaka 2005, 2006, 2007, 2015, 2017, 2018 na 2019.

Kwingineko, timu ya Kisumu iliibuka mshindi wa Ligi ya Daraja ya Pili baada ya kuchabanga Western Bulls 23-5 katika fainali uwanjani Kakamega Showground.

Timu hizo mbili zitashiriki Ligi Kuu ya msimu 2019-2020 baada ya kujikatia tiketi ya kurejea katika ligi ya daraja ya juu wiki moja iliyopita ziliposhinda mechi zao za nusu-fainali.

Bulls kutoka Kaunti ya Kakamega ilipiga Chuo Kikuu cha USIU kutoka Nairobi kwa alama 22-16 nayo Kisumu ikalemea Catholic Monks pia kutoka Nairobi, 14-11.

Bulls na Kisumu zilitemwa kutoka Ligi Kuu msimu 2016-2017 na 2013-2014, mtawalia.

Mnamo Ijumaa, Kisumu ililemea Bulls kupitia miguso ya Boniface Okoth, Denver Audo, Moses Amonde na Jaycox Mavala na penalti kutoka kwa Lenny Obiero.

Allan Kasiti alifungia Bulls mguso wa kufutia machozi sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kilie. Nayo KCB Cubs ilihifadhi ubingwa wa kipute cha Eric Shirley Shield kwa kunyuka Homeboyz 11-5.

Historia kati ya KCB na Kabras Sugar kwenye Kenya Cup

Novemba 8, 2014: KCB 13-3 Kabras (msimu wa kawaida)

Machi 14, 2015: KCB 27-3 Kabras (fainali)

Desemba 19, 2015: KCB 40-15 Kabras (msimu wa kawaida)

Desemba 3, 2016: Kabras 15-15 KCB (msimu wa kawaida)

Aprili 22, 2017: KCB 36-8 Kabras (fainali)

Februari 24, 2018: KCB 41-12 Kabras (msimu wa kawaida)

Machi 24, 2018: KCB 29-24 Kabras (fainali)

Februari 23, 2019: KCB 44-20 Kabras (msimu wa kawaida)

Mei 18, 2019: Kabras Sugar 15-23 KCB (fainali)