Michezo

Kenya Harlequins kutangaza kocha mpya baada ya mchakato wa kutafuta mrithi wa Habimana kukamilika

June 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Ligi Kuu ya raga ya humu nchini, Kenya Harlequins kinatarajiwa kufichua kocha mpya wiki ijayo.

Mwenyekiti Michael Wanjala amethibitisha kuwa mchakato wa kumtafuta mkufunzi mpya atakayemrithi Dominique Habimana umekamilika baada ya makocha wanane waliotuma maombi ya kazi kufanyiwa mahojiano.

Jopo lililoteuliwa na Harlequins kuongoza mahojiano hayo lilijumuisha mkufunzi wa sasa wa Kenya Simbas Paul Odera, Gordon Anampiu aliyewahi kunoa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa na mkuu wa kamati ya kiufundi ya Harlequins, Victor Sudi.

“Hili ni jopo linalojivunia uelewa wa kina kuhusu raga ya humu nchini na ya kimataifa. Watakuwa na usemi wa mwisho kuhusu kocha mpya wa Harlequins,” akasema Wanjala.

Nafasi ya kocha kambini mwa Harlequins ilisalia wazi mwanzoni mwa mwezi huu baada ya Habimana aliyekuwa amedhibiti mikoba yao kwa msimu mmoja pekee kusimamishwa na kushauriwa kutuma upya maombi ya kazi.

Mbali na kuwanoa Kenya Simbas kwa kipindi kirefu, Habimana amewahi pia kuwaongoza Nakuru RFC kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Raga ya Kenya Cup mnamo 2013 na 2014.

Ingawa hivyo, mbinu zake za ukufunzi hazikufaulu msimu huu baada ya kushuhudia Harlequins ambao ni mabingwa mara nane wa Ligi Kuu ya Kenya Cup wakiambulia nafasi ya tisa kwenye jedwali la kipute hicho na hivyo kukosa kufuzu kwa mchujo.

Kwa mtazamo wa Wanjala, matokeo duni ya kikosi chake ni maandalizi mabaya yaliyochangiwa na ukosefu wa mdhamini kabla ya mwanzo wa kampeni za msimu huu.

Ameshikilia kwamba usimamizi wa Harlequins kwa sasa unapania kuimarisha zaidi benchi ya kiufundi hasa baada ya kutangaza pia nafasi za kazi kwa kocha wa akademia na mkufunzi wa mazoezi ya viungo vya mwili.

Harlequins ambao wanajivunia kutoa wanaraga matata ambao wamekuwa wakiviwajibikia vikosi vya kitaifa vya Shujaa, Simbas na Chipu, tayari wameanza mpango wa kujifua kwa minajili ya msimu ujao.

Kufikia sasa, wamefaulu kuwasajili wanaraga Mark Wandetto kutoka Homeboyz na Leroy Mbugua wa Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Baadhi ya chipukizi ambao Harlquins wanalenga kuwakweza kutoka akademia hadi kikosi cha kwanza ni nahodha wa kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 20 Boniface Ochieng, Elisha Koronya na Melvin Thairu waliokuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Kenya Simbas mnamo 2019.

Katika kivumbi cha msimu huu, Harlequins walisajili ushindi katika mechi tano na kupoteza jumla ya michuano 11 katika matokeo yaliyowashuhudia wakijizolea alama 28 pekee.