Kenya hatarini kunyimwa mikopo kufuatia deni la Sh7 trilioni

Kenya hatarini kunyimwa mikopo kufuatia deni la Sh7 trilioni

DAVID MWERE Na BENSON MATHEKA

Huenda ikawa vigumu kwa Kenya kukopa kutoka mashirika ya wafadhili duniani kutokana na deni linaloendelea kuongezeka. Wataalamu wa uchumi katika Bunge la Kitaifa wanaonya kuwa, huenda ikawa vigumu Kenya kukopa pesa kutoka mashirika hayo siku zijazo.

Hii ni baada ya ripoti ya bunge hilo kuonyesha kuwa deni la taifa linakadiriwa kuwa Sh9 trilioni katika muda wa miaka mitatu ijayo.

“Kuna haja ya kutumia fedha za mkopo kwenye miradi inayofaa wananchi ndipo waridhike kuwa pesa hizo huwa hazifujwi. Pia uwekezaji wa pesa hizo ni muhimu japo mwanya wa kukopa kutoka mashirika ya kimataifa unaendelea kupungua,” ikasisitiza ripoti hiyo.

Inasema deni la taifa linatarajiwa kuwa Sh7.5 trilioni kufikia Juni, 2021. Ripoti ya Afisi ya Bajeti Bungeni (PBO) inaonya kwamba, kutokana na matumizi mengi ya serikali, deni la taifa huenda likapanda na kufikia Sh9.2 trilioni kufikia mwaka wa kifedha wa 2022/23.

Mwaka huu matumizi ya fedha za serikali ambazo ni Sh873 bilioni, yalitokana na gharama kubwa ya miradi inayofadhiliwa pamoja na kupungua kwa mapato yanayotokana na ushuru.

Miaka ya nyuma, fedha zinazotumika zimekuwa zikipanda kwa kuwa kiasi kikubwa huelekezwa kwenye miradi ya kujenga miundombinu, uzalishaji wa kawi na miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na serikali.

“Athari ya virusi vya corona kwenye uchumi wetu ni dhahiri hasa kimapato mwaka huu wa kifedha 2020/21,” ikasema ripoti hiyo.

Serikali nayo huenda ikalazimika kukopa fedha zaidi huku athari ya janga la virusi vya corona ikiendelea kushuhudiwa nchini na mataifa mengine duniani.

Kulingana na ripoti hiyo, fedha ambazo zitaelekezwa katika ulipaji wa madeni zinatarajiwa kupanda na kuchukua asilimia 49 ya mapato yote ya nchi mwaka huu wa kifedha.

“Hii inamaanisha kwamba, asilimia 51 pekee ya mapato ya nchi itaelekezwa kwenye utekelezaji wa bajeti ya 2020/21,” ikaongeza ripoti ya PBO.Mwaka huu wa kifedha, serikali inapanga kutumia Sh3.2 trilioni baada ya kuangazia upya bajeti ya Sh2.79 trilioni iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Ukur Yattani bungeni mnamo Juni.

Hii sio mara ya kwanza kwa wataalamu kuonya kuwa madeni ya serikali ya Jubilee yataathiri uchumi wa nchi. Hata hivyo, serikali imekuwa ikitetea madeni ikisema kuwa inatumia pesa inazokopa kuimarisha miundo misingi.

You can share this post!

Alex Song aliyewahi kutamba Arsenal na Barcelona asajiliwa...

Simanzi vijana watano marafiki wakiangamia ajalini