KENYA HIGH JUU

KENYA HIGH JUU

Na WANDERI KAMAU

SHULE ya Upili ya Wasichana ya Kenya High, katika Kaunti ya Nairobi, jana iliibuka ya kwanza kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita, kwa kupata alama 10.76.

Shule hiyo iliendelea kuonyesha ubabe wake kwenye mtihani huo kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kung’aa tena nchini 2019, kwa kupata alama ya wastani ya 10.47.

Shule hiyo ilifuatwa na Alliance Girls, Kapsabet Boys, Maranda High School, Machakos Girls, Mang’u Boys, Kaaga Girls, Alliance Boys, Agoro Sare Boys na Chanda Boys.

Shule ya Kapsabet Boys ilishuka kwa kushikilia nafasi ya tatu mwaka uliopita, ikilinganishwa na 2019, ambapo iliorodheshwa ya pili.

Kwenye matokeo hayo yaliyotolewa jana na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha, mwanafunzi Simiyu Robin Wanjala kutoka Shule ya Murang’a High aliibuka bora nchini kwa kuzoa alama ‘A’ ya pointi 87.344. Shule zilizokosa kuwika mwaka huu licha ya kuwa miongoni mwa shule kumi bora nchini 2019 ni Kisima Mixed, MaryHill Girls, Strathmore School na Moi High School, Kabarak.

Akitangaza matokeo hayo, waziri alisema yaliimarika pakubwa licha ya wanafunzi kuufanya mtihani huo chini ya mazingira magumu kutokana na janga la virusi vya Corona.

Wanafunzi 893 walipata alama ya ‘A’, 6,420 (A-), 14 427 (B+), 25, 207 (B-) na 57,999 (C+).

Kijumla, wanafunzi 143,140 walipata alama ya C+ kwenda juu, na hivyo kujishindia nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu vya umma. Mnamo 2019, wanafunzi 627 ndio walifanikiwa kupata alama ya ‘A.’

Kwenye mtihani huo, matokeo ya masomo 19 yaliimarika, ikilinganishwa na 2019, ambapo ni matokeo ya masomo 16 yaliyoimarika. Hakukuwa na mabadiliko yoyote kwenye matokeo ya masomo mawili.

Miongoni mwa wale waliokuwepo kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kuwajiri Walimu (TSC), Bi Nancy Macharia, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, Bi Mercy Karogo, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, Bi Florence Mutua (aliye Mwakilishi wa Wanawake, Busia) kati ya wengine.

Bi Macharia aliwashukuru walimu kwa kujitolea pakubwa kusimamia mtihani huo licha ya wengi wao kuathiriwa na virusi vya corona.

Alisema kuwa kufikia sasa, walimu 151,494 wamepewa chanjo dhidi ya virusi hivyo, hilo likiwa karibu nusu ya walimu kote nchini.

Kama mtangulizi wake Dkt Fred Matiang’i, Prof Magoha alitoa matokeo hayo bila ya mbwembwe na matumbuizo kutoka kwa kwaya mbalimbali, kama ilivyokuwa miaka ya awali.

You can share this post!

Ratiba ya Kenya Simbas ya Kombe la Afrika 2021 ya kuingia...

FAUSTINE NGILA: Jihadhari na matapeli wa sarafu za...