Kenya ilipoteza Sh560 billioni kutokana na corona  2020 – Rais Kenyatta

Kenya ilipoteza Sh560 billioni kutokana na corona 2020 – Rais Kenyatta

 

Na SAMMY WAWERU

KENYA ilikadiria hasara ya Sh560 bilioni katika ukuaji wa uchumi mwaka uliopita, 2020 kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini. Kisa cha kwanza cha virusi vya corona kiliripotiwa Machi 13.

Jumamosi iliyopita, Kenya iliadhimisha mwaka mmoja tangu ithibitishe kuwa mwenyeji wa janga hili ambalo sasa ni kero la kimataifa.

Kwenye hotuba yake kwa taifa majuzi, Rais Uhuru Kenyatta alisema uchumi ulitarajiwa kukua kwa asilimia 6 ila hilo halikuwezekana kwa sababu ya Homa ya Corona.

“Uchumi ulitarajiwa kukua kwa asilimia 6 mwaka uliopita, 2020 ila ulikua kwa asilimia 0.6,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi huyo wa nchi hata hivyo alieleza matumaini na imani kwamba mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kufufua uchumi itaufanikisha kukua kwa asilimia 7, kufikia mwishoni mwa mwaka ujao, 2022.

Rais Kenyatta alisema lengo la serikali ni kuona uchumi umefufuka na kuboreka, na ndio sababu haikukaza kamba sheria na mikakati kama ilivyotarajiwa na wengi kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya corona.

Katika siku za hivi karibuni taifa limeshuhudia ongezeko la visa vya maambukizi yanayoandikishwa kila siku na pia idadi ya wanaongamizwa na virusi vya corona.

“Hatujafunga uchumi kwa sababu tunataka ukue. Uchumi wetu waweza kufufuka ila tunahitaji kuwa macho sana. Hata wakati tunaendelea kuushughulikia muhimu zaidi ni maisha ya Wakenya, lazima tuchukue tahadhari,” akafafanua Rais Kenyatta, akihimiza Wakenya kutilia mkazo sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kusaidia kuzuia msambao zaidi.

Sekta mbalimbali zimeathirika baada ya Kenya kukumbwa na ugonjwa wa Covid-19.

Mamia na maelfu ya watu walipoteza kazi mwaka uliopita, kutokana na makali ya corona ambayo yaliyumbisha uchumi.

You can share this post!

Kinadada wa Kenya wafundisha wenzao kutoka Uganda jinsi ya...

Vitambulisho vya kitaifa kufutiliwa mbali, Huduma Namba...