Michezo

Kenya ilipoteza wasaa kushiriki mbio za mita 10,000 Nigeria

August 2nd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kupata medali katika mbio za mita 10, 000 za wanaume katika kila makala ya Riadha za Bara Afrika tangu mwaka 2010, Kenya iliandikisha matokeo duni katika kitengo hiki ilipotoka mikono mitupu mjini Asaba nchini Nigeria hapo Agosti 1, 2018.

Waethiopia Jemal Yimer Mekkonen na Andamlak Belihu Berta walichukua nishani za dhahabu na fedha kwa dakika 29:08.01 na 29:11.09, mtawalia. Mganda Timothy Toroitoch alihakikisha Kenya inaambulia pakavu hapa alipompiku Vincent Kipsang’ na kunyakua shaba kwa dakika 29:11.87.

Kipsang’, ambaye aliongoza mbio hizi za mizunguko 25 kwa kipindi kirefu kabla ya kuishiwa pumzi kengele ilipolia, alimaliza katika nafasi ya nne (29:14.52).

Mara ya mwisho Kenya haikushinda medali katika kitengo hiki ni mwaka 2008. Ilizoa dhahabu na shaba kupitia kwa Wilson Kiprop na Geoffrey Mutai jijini Nairobi mwaka 2010, mtawalia. Kenya ilifagia medali zote katika makala ya mwaka 2012 jijini Porto-Novo nchini Benin kupitia kwa Kenneth Kipkemoi, Mark Kiptoo na Lewis Mosoti, mtawalia.

Josphat Bett alishindia Kenya nishani ya shaba mjini Marrakech nchini Morocco mwaka 2014 naye Wilfred Kimitei akanyakua medali ya fedha katika makala yaliyopita mjini Durban nchini Afrika Kusini mwaka 2016.

Riadha za Afrika za mwaka 2018 zinaandaliwa uwanjani Stephen Keshi mjini Asaba kutoka Agosti 1-5. Kenya inawakilishwa na wanariadha 65.