Habari

KENYA IMARA: Mashujaa walivyowazidi nguvu magaidi

January 17th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameibuka mashujaa na imara zaidi kama taifa, kufuatia shambulizi la kigaidi mnamo Jumanne katika majengo ya hoteli ya Dusit D2 jijini Nairobi kwa kuwafagilia majambazi waliolenga kuleta maafa ya mauaji, uharibifu wa mali na taharuki.

Shambulizi hilo lilidhihirisha nguvu kuu ya Kenya katika kusimama imara na kulinda uhuru wa nchi yao.

Magaidi hao wanaokisiwa kuwa sita waliuawa kwenye operesheni ambayo imepokea sifa kimataifa kutokana na ushujaa wa maafisa wa usalama na raia waliohusika katika shughuli za uokoaji na kukabiliana na wavamizi hao.

Magaidi hao walivamia hoteli hiyo mwendo wa saa tisa Jumanne alasiri wakilenga kuua raia wasio na hatia kwenye kampeni yao potovu. Lakini maafisa wa usalama wa Kenya kutoka vikosi mbalimbali na waokoaji waliibuka mashujaa kwa kukomesha juhudi za magaidi hao.

Vikosi maalum vikijumuisha Recce, RDU, Flying Squad na kile cha KDF vilidhihirisha uwezo wa Kenya kukabiliana na hatari yoyote.

Maafisa hao walifika kwa haraka katika eneo la tukio na mara moja wakaanza juhudi za kuokoa raia waliokuwa wamekwama katika hoteli hiyo na majengo yaliyo karibu, huku wakikabiliana vikali na magaidi walioua watu 14 na kujeruhi wengine kadhaa.

Hali ingekuwa mbaya zaidi kama sio juhudi za maafisa hao za kufika hapo kwa haraka, pamoja na kutekeleza shughuli hiyo kwa utaalamu mkubwa bila uwoga.

Maafisa hao walifanikiwa kunusuru watu zaidi ya 700 na kufikia jana asubuhi walikuwa wamewaua wavamizi wote.

Maafisa wa polisi wa kawaida, GSU na AP pia walitekeleza wajibu muhimu katika operesheni hiyo ya kipekee kwa kuweka usalama mkali nje ya majengo hayo, kudhibiti raia, kusaidia katika kufanikisha manusura kupelekwa hospitalini na kuwahoji waliookolewa.

Wakiandika kwenye mitandao ya kijamii, Wakenya wengi walitambua mahsusi juhudi za maafisa wa kikosi cha Recce, ambacho kina mafunzo maalum ya kukabiliana na hatari. Ni maafisa wa kikosi hicho waliotangulia kuingia katika jengo hilo na kuwaokoa raia waliokuwa katika hatari ya kuuawa na magaidi hao.

Mbali na kuwasili eneo la shambulizi kwa haraka, maafisa wa usalama walielewana vyema tofauti na walivyoshughulikia shambulizi la Westgate ambapo watu 67 waliuawa na la Chuo Kikuu cha Garissa ambapo147 walipoteza uhai.

Juhudi za maafisa wa usalama zilitambuliwa na Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika Mousa, Faki Mahamat aliyesifu maafisa wa usalama wa Kenya kwa kuchukua hatua za haraka kukabili shambulizi hilo.

Balozi wa Amerika nchini Robert Godec alitaja hatua ya maafisa wa usalama wa Kenya kama ya kijasiri.

Wakenya wanaoishi Canada na Amerika pia walipongeza maafisa wa usalama wa Kenya kwa kuchukua hatua ya haraka.

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi ambaye mwanawe aliokolewa kutoka eneo la shambulizi pia walisifu maafisa wa usalama.

Raia pia walijitolea mhanga katika kudunisha mipango ya magaidi walipohatarisha maisha yao kuokoa watu. Mmoja wao ni Inayat Kassam, ambaye alionekana akiingia mara kadhaa katika hoteli hiyo kuwaokoa watu bila kuvalia magwanda ya kujikinga risasi.

Picha za Bw Kassam zilienezwa mitandaoni zikiambatishwa na jumbe za kumpongeza huku Wakenya wakitaka atuzwe kama shujaa wa kitaifa.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Kassam kuonyesha ujasiri wa aina yake. Magaidi waliposhambulia jumba la kibiashara la Westgate, Nairobi mnamo 2014 alikuwa msitari wa mbele kuwaokoa raia.

Maafisa wa uokoaji wakiongozwa na Shirika la Msalaba Mwekundu na madereva wa ambulensi nao walichangia pakubwa katika shughuli hiyo kwa juhudi zao za kuwapatia majeruhi huduma ya kwanza na kuhakikisha wamepelekwa hospitalini, pamoja na kuwashauri walionusurika.

Juhudi hizo zilisaidia kuokoa maisha na kupunguza mishtuko miongoni mwa waliookolewa.