Habari MsetoKimataifa

Kenya imepiga hatua kubwa za ugatuzi – Balozi wa Ujerumani

October 15th, 2018 2 min read

Na AGGREY MUTAMBO

BALOZI mpya wa Ujerumani nchini Kenya, Bi Annett Günther, amesema ugatuzi utasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mbali kutoka mijini kuboresha hali yao ya kimaisha.

Hata hivyo, alikiri kuwa huenda Wakenya wakaendelea kukumbwa na changamoto ambazo zitapungua jinsi muda unavyosonga.

“Kwa muda mfupi ambao nimekuwa humu nchini, na wale watu nimekutana nao, ninaweza kuona kwamba wote wanasisitiza kuhusu manufaa ambayo kaunti zimepata kutokana na ugatuzi na kuna hatua kubwa ambazo zimetekelezwa,” akasema.

Balozi huyo alisema hayo katika mahojiano baada ya kukutana na Gavana wa Kisumu, Prof Anyang Nyong’o, kabla ya kuzuru Kaunti ya Kakamega.

“Nadhani kwa kipindi cha miaka mitano pekee, kumekuwa na hatua kubwa zilizopatikana katika uongozi,” akaongeza balozi huyo ambaye aliwasili nchini miezi mitano iliyopita.

Serikali 47 za ugatuzi Kenya, zilizoundwa 2013 baada ya katiba mpya kupitishwa 2010, zinafaa kuwa serikali ndogo za kuleta huduma bora za umma karibu na wananchi.

Lakini changamoto ambazo zimeonekana kufikia sasa zinahusu jinsi ya kushirikiana na serikali kuu, mbinu za kujikusanyia fedha na kiwango cha fedha ambacho serikali kuu inafaa kutuma mashinani kutoka kwa Wizara ya Fedha.

Kwenye Sheria ya Fedha 2018, wizara ya Fedha ilipunguza kiwango cha mgao wa fedha za kaunti kwa Sh9 bilioni ikilalamikia uhaba wa pesa za umma, licha ya malalamishi kutoka kwa magavana.

Wakati Kenya ilipopata uhuru 1963, Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kutambua taifa hili ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na serikali mpya ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Kwa sasa kuna karibu kampuni 120 za Ujerumani nchini Kenya, ambazo hutoa ajira kwa takriban watu 4,500.

Nchi hiyo inaendeleza mashauriano na serikali kuanzisha mpango maalumu wa mafunzo ya kiufundi kwa vijana ili kuchangia kwa mafanikio ya ajenda nne za maendeleo hasa kuhusu uzalishaji wa bidhaa.

“Nchini Ujerumani tumekuwa na mfumo wa ugatuzi kwa zaidi ya miaka 70 na tukitazama nyuma, tunajua inaweza kuchukua muda mrefu kutekeleza mfumo huu kikamilifu,” akasema.

Aliongeza kuwa changamoto zilizopo zinaweza kutatuliwa.