KENYA IMESOTA!

KENYA IMESOTA!

LEONARD ONYANGO Na BENSON MATHEKA

SERIKALI sasa inategemea mikopo kuendesha shughuli zake baada ya kuishiwa na fedha kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa kifedha (2020/2021) Juni 30, 2021.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani kwenye Gazeti Rasmi la Serikali, Kenya ilikuwa imesalia na Sh2.4 bilioni pekee kufikia Mei 31, mwaka huu.

Hiyo inamaanisha kwamba, serikali haikuwa na fedha za kuendeshea shughuli zake kuanzia Juni 1, mwaka huu.

Mamlaka ya Ushuru (KRA) ilikusanya Sh1.3 trilioni na Wizara ya Fedha ilikopa Sh894 bilioni; Sh770 bilioni kutoka taasisi za kifedha za humu nchini na Sh124 bilioni kutoka mataifa ya kigeni.

Hiyo inamaanisha kwamba, kila Sh100 zilizokusanywa na KRA, Sh59 zilitumika kulipa madeni na kusalia na Sh41 kulipa mishahara, pensheni, marupurupu ya watumishi wa serikali na miradi ya maendeleo.

Pia inamaanisha kwamba, Kenya ilikopa Sh2.6 bilioni kila siku kati ya Julai 1, 2020 na Mei 31, mwaka huu, kuendesha shughuli zake.

Ripoti hiyo ya Wizara ya Fedha inaonyesha kuwa, jumla ya Sh899.6 bilioni zilitumiwa katika kulipa madeni, mishahara, kukarabati magari ya watumishi wa serikali, kununua mafuta, kulipa pesheni na marupurupu.

Fedha zilizotumiwa katika maendeleo ni Sh286 bilioni pekee.

Serikali za Kaunti zilipokea Sh263.5 bilioni kati ya Sh383 bilioni zilizokuwa zimetengwa na Hazina Kuu ya Kitaifa.

Kenya iliwekwa katika orodha ya mataifa yaliyo katika hatari kubwa ya kushindwa kulipa madeni mnamo 2020.

Serikali inalenga kuokoa Sh82 bilioni ambazo zingetumika kulipa nyongeza ya mishahara.

Tayari, serikali kupitia tume ya kutathmini mishahara ya watumishi wa umma imetangaza kusitisha nyongeza ya mishahara kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyosababishwa na mkurupuko wa ugonjwa wa Corona.

Hatua hiyo inatokana na maafikiano kati ya serikali na Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF) ambapo Kenya ilikubali kusitisha nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma na kuajiri wafanyakazi wapya hadi 2025.

Serikali pia imeshindwa kulipa vijana ambao wamekuwa wakishiriki mpango wa Kazi Mtaani.

Katibu Mkuu wa Idara ya Makazi na Ustawi wa Miji, Charles Hinga, jana alisema wizara inangojea fedha kutoka kwa Hazina Kuu ili kuwalipa vijana walioshiriki katika awamu ya pili ya mpango huo ulioanzishwa Aprili 2020 kuwezesha vijana kujikimu kimaisha kufuatia makali ya janga la Corona.

Awamu ya pili ya Kazi Mtaani ilianza Julai 2020 ambapo vijana 280,000 walishiriki katika kudumisha usafi katika mitaa ya mabanda kwenye kaunti zote 47. Kila kijana alilipwa wastani wa Sh600 kwa siku. Vijana 310,000 walishiriki awamu ya kwanza ya Kazi Mtaani iliyoanza Aprili 2020 na kumalizika Juni, mwaka jana.

Mwenyekiti wa Mabunge ya Kaunti Wahome Ndegwa alisema madiwani hawajapata marupurupu yao kama vile kuhudhuria vikao na fedha za mafuta ya magari tangu Februari mwaka huu.

“Madiwani wanapata mishahara kama kawaida lakini tatizo ni marupurupu hatujakuwa tukipata. Vilevile, miradi ambayo imekuwa ikifanywa na mabunge ya kaunti kama vile ukarabati wa kumbi za vikao, imekwama kutokana na ukosefu wa fedha,” Bw Ndegwa akaambia Taifa Leo.

Wabunge pia hawajapokea fedha za CDF ikisalia wiki moja kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa fedha,” akasema mbunge wa Machakos mjini, Dkt Victor Munyaka.

Mbunge huyo alisema kufikia sasa, Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF) imepokea asilimia 75 ya mgao wao.

“Kwa kawaida fedha za NG-CDF huwa zinatolewa miezi kadhaa kabla kukamilika kwa mwaka wa fedha. Lakini sasa tumesalia na wiki moja na hatujapata fedha. Hiyo ni ishara kwamba serikali ‘imesota’,” akasema.

Kila eneobunge linastahili kupokea Sh137 milioni kwa ajili ya hazina ya NG-CDF.

Mnamo Jumanne wiki hii, Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliambia kamati ya seneti kwamba, Kenya inakabiliwa na hali mbaya kifedha.

“Tuna changamoto ya ukusanyaji ushuru kutokana na hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na janga la corona. Tunatatizika kutoa pesa kwa wizara, idara na mashirika ya serikali pia,” alisema Bw Yatani.

Alisema hali hii imeathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Ninataka kuwathibitishia kwamba, ilivyo leo, vyanzo vyetu vya fedha na njia kadhaa hazijafunguka,” aliiambia kamati inayosimamiwa na seneta wa Kirinyaga, Charles Kibiru.

Magavana wametishia kusitisha shughuli katika kaunti zote kutokana na ukosefu wa fedha.

Magavana mapema wiki hii walitoa makataa ya siku 10 kwa Hazina Kuu ya Kitaifa kutoa Sh102.6 bilioni, la sivyo huduma zote zitasitishwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora alisema ukosefu wa fedha umetatiza utoaji wa huduma muhimu katika Kaunti.

Kenya Alhamisi, ilithibitisha kupokea mkopo wa Sh108 bilioni wa Eurobond kufadhili bajeti yake ya 2021/2022. Wiki iliyopita, Kenya pia ilipokea mkopo wa Sh80.9 bilioni kutoka kwa Benki ya Dunia.

Mnamo Alhamisi, Benki ya Dunia ilisema itaondoa Kenya katika orodha hiyo 2028 iwapo serikali itafuata mwongozo wa kupunguza matumizi uliotolewa na taasisi hiyo ya kifedha.

“Kwa sasa, tunakopa hapa kulipa pale, hii sio salama kwa nchi,” mtaalamu wa masuala ya uchumi Kamwe Owino alisema akichanganua bajeti ya mwaka huu.

You can share this post!

Daktari wa KNH aliyejiua kuzikwa habari zaidi zikiibuka

Nassir na Shahbal walilia ‘tosha’ ya Raila...