Habari

Kenya ina uwezo wa kulipa madeni yake – Wizara ya Fedha

March 20th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

WIZARA ya Fedha imekariri- kuwa nchi ina uwezo wa kulipa deni lake lote, na kuwa kuna mwanya mkubwa unaoruhusu serikali kukopa fedha zaidi.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Sera kuhusu Usimamizi wa Madeni na Udhibiti wa Mikasa  kwenye wizara hiyo, Bw Daniel Ndolo, ameiondolea serikali lawama kuhusu madai ya kukopa kiholela akisema ni Bunge la kitaifa linalowapa ruhusa ya kutafuta fedha za kugharamia miradi mbalimbali kupitia mikopo.

Kauli yake inawiana na ile aliyotoa majuzi Waziri wa Fedha Henry Rotich kwamba kiwango cha deni la nchi ni cha chini kikilinganishwa na mapato yake.

Kwa sasa Kenya inadaiwa Sh4.6 trillioni ambazo ni asilimia 54 ya mapato ya nchi, na kulingana na Bw Ndolo kiwango hicho kinatarajiwa kufikia asililimia 59 mwaka wa kifedha wa 2018-2019 iwapo mkopo zaidi itachukuliwa.

“Serikali kukopa fedha si jambo baya ila swali muhimu ni kama ina uwezo wa kulipa deni lake na kama fedha hizo zinatumika kwa miradi lengwa badala ya kufujwa kupita sakata za ufisadi,”  akasema.

Afisa huyo aliyasema hayo kwenye kongamano la siku moja lililoandaliwa na Muungano wa KARA (Kenya Alliance of Residential Association) hoteli ya Panafric ambapo alimwakilisha Katibu wa Wizara Kamau Thugge.

Hata hivyo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Dkt X.N Iraki alitofautiana na mwanauchumi huyo na kusema kwamba hata wataalamu wa maswala ya fedha kutoka mataifa ya nje mara si moja wamehoji uwezo wa serikali kulipa deni linalodaiwa.

“Mikopo kama Eurobond hatujaona manufaa yake na baadhi ya miradi inayodaiwa kufadhiliwa na pesa hizo hazijafaulu.Mlipa kodi atatwika jukumu zito la kulipa pesa hizo tukiendelea kukopa zaidi,” akasisitiza.

Mshauri wa maswala ya kifedha Ndirangu Ngunjiri alisema kwamba uchumi wa serikali hauwezi kustahimili ukopaji wa nyumbani lakini akaongeza kwamba hiyo siyo sababu tosha ya serikali kukumbatia mikopo kiholela kutoka mataifa ya nje.

Kilichojitokeza bayana kwenye kongamano hilo ni kauli za kupinga nia ya serikali ya kuendelea kukopa huku washiriki wakisema nchi ingewajibikia vizuri mikopo ya awali basi  hata ruwaza ya 2030 ingekuwa imefanikishwa.

Mwenyekiti wa Shirika hilo Richard Nyaga na washiriki kutoka mashirika mbalimbali walihudhuria kongamano hilo.