Habari Mseto

'Kenya ina watoto wa mitaani zaidi ya 46,000'

June 12th, 2020 1 min read

NA STEVE OTIENO

Sensa ya kitaifa iliyofanywa hapo 2019 imefichua kwamba Kenya ina watoto wa mitaani zaidi ya 46,000.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa kwa umma kwa mara ya kwanza majuzi na Waziri wa Leba na Usalama wa Kijamii Bw Simon Chelugui ilitokana na mradi ulioanzishwa na Hazina ya Watoto wa Mitaani iliyoanzishwa Machi 11, 2003 kushughulikia maswala ya chokoraa mijini.

Ripoti hiyo pia ilihusisha Shirika la Kitaifa la Twakimu nchini (KNBS) na UNICEF.

“Takwimu tulizo nazo hapa zitatusaindia kukabiliana na matatizo yanayowakumba chokoraa katika miji mbalimbali,” alisema waziri huyo.

Baadhi ya matatizo yanayokumba familia za mitaani ni ukosefu wa matibabu bora, uhaba wa chakula, dhuluma na kukosa makazi bora.

Bw Chelugui alisema kwamba Sh144 milioni zimetengwa ili kushughulikia maswala ya familia hizo.

“Kutokana na changamoto wanazopitia, tunajizatiti kushirikiana na washikadau wote kutumia takwimu hizi kubuni mikakati na sulushu kwa familia hizi,” meneja wa KNBS Robert Buluma alisema.