Habari

Kenya inahitaji Sh167 bilioni kukabili baa la njaa – Ripoti

November 1st, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI inahitaji kitita cha Sh167 bilioni ili kuweza kutekeleza mpango unaolenga kuwezesha Kenya kuwa na chakula cha kutosha kufikia 2027.

Kulingana na Mwongozo wa Utekelezwaji wa Mpango wa Kilimo cha Kisasa kati ya 2018-2027, serikali ya kitaifa pia itahitaji kushirikiana na serikali za kaunti ili kuweza kuzalisha chakula cha kutosha na kuangamiza njaa ambayo inasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwongozo huo ulizinduliwa Jumatano katika makao makuu ya wizara ya Kilimo jijini Nairobi.

Katibu Msimamizi wa wizara ya Kilimo

Andrew Tuimur alisema serikali imetambua hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa Kenya inajipatia chakula cha kutosha kufikia 2022, kulingana na Malengo Makuu Manne ya Miradi ya Maendeleo ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Miongoni mwa hatua hizo ni kuwekeza katika upanuzi wa mashamba ya kilimo cha unyunyiziaji maji, kubuni hazina ya utafiti wa kilimo cha kisasa na kuwahimiza wakulima wa mashamba madogo kutumia teknolojia za kisasa katika ukulima,” akasema Dkt Tuimur.

“Serikali pia itatoa vifaa vya kuhifadhia mazao kwa wakulima ili kuhakikisha kwamba wakulima hawapati hasara baada ya kuvuna,” akaongezea.

Kulingana na mwongozo huo, serikali pia inalenga kuanzisha bima ya mazao, mifugo na uvuvi ili kuwalipa fidia wanapokumbwa na mikasa inayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile ukame na mafuriko.

“Kuanzia sasa wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na washikadau wengineo wataanza kuhamasisha Wakenya kuhusiana na yaliyomo katika mwongozo huo,” akasema.

Alisema serikali inalenga kupata fedha za kufadhili mpango huo kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayokabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwakilishi wa Shirika la Kilimo Duniani (FAO) humu nchini Gabriel Rugalema alisema Umoja wa Mataifa (UN) tayari umetoa msaada wa Sh300 milioni ili kusaidia kufanikisha mwongozo huo.

“Shirika la FAO litashirikiana na Kenya kuhakikisha kuwa mpango wa kutekeleza kilimo cha kisasa unatekelezwa kikamilifu,” akasema.

Kuwezesha Kenya kuzalisha chakula cha kutosha ni miongoni mwa miradi mikuu minne ambayo Rais Kenyatta analenga kutekeleza kabla ya kustaafu 2022.

Sekta ya Kilimo huchangia asilimia 25 ya mapato ya Kenya moja kwa moja.

Kulingana na takwimu za wizara ya Kilimo Kenya huenda ikapoteza asilimia 3 ya mapato yake endapo haitachukua hatua mwafaka kukabiliana na makali ya mabadiliko ya hewa kufikia 2030.