Habari

Kenya itaendelea kulinda mipaka yake kwa dhati – Monica Juma

February 23rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA
 
KENYA haitaruhusu kutwaliwa hata kwa nukta moja ya himaya yake katike eneo la mpaka katika habari hindi ambayo ndio chanzo cha mzozo kati yake na taifa la Somalia, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Monica Juma amesema.
Dkt Juma alisema hayo Alhamisi jioni huku Somali ikisubiri kujibu malalamishi ya Kenya kuhusiana na uamuzi wake wa kuuza maeneo yenye utajiri wa mafuta na gesi katika eneo la mpaka ambalo linazozaniwa katika habari Hindi.
Uamuzi huo uliafikiwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta jijini Nairobi.
Mkutano huo ambao ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi pia ulijadili na kukubaliana kuhusu mwongozo wa kutatua mizozo na kulinda himaya ya Kenya, rasilimali zake za majini zikiwemo mafuta na gesi na ukubwa wa eneo la Bahari Hindi ambao uko ndani ya Kenya.
Akiongea na wahabari katika Hoteli ya Intercontinental baada ya kukutana na wabunge wanachama wa Kamati kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni, Dkt Juma majibu ya Somalia kuhusu suala hilo hayakuridhisha Kenya.
“Tulituma barua ya malalamishi Somalia mnamo Februari 9, tulipogundua kwamba Wizara ya Mafuta na Madini ya Somalia imenadi maeneo hayo jijini London,” Dkt Juma, ambaye alikuwa ameandamana na Katiba wa Wizara hiyo Macharia Kamau, akasema.
“Kwanza tulimwita balozi wa Somalia ili afafanua kile ambacho serikali yake ilifanya. Alisema kuwa hakuwa na habari, hatua iliyotulazimisha kumtuma nchini mwake ili asaka habari tuliyotaka. Na aliporejea bado alisema hakuwa na habari,” akaongeza Dkt Juma.
Kenya inataka Somalia kuondoa madai kuwa eneo hilo liko katika himaya yake, isitishe mnada huo na itambue mipaka ya kati ya mataifa hayo mawili ya tangu ukoloni.

Lakini huku Kenya ikilamika, Taifa Leo Dijitali imebaini kuwa mchakato wa kunadi maeneo hayo yenye mafuta na gesi katika bahari Hindi unaendelea na kipindi cha kutangaza ununuzi kinafaa kukamilika Septemba mwaka huu.

Mnunuzi atakaoibuka mshindi atatangazwa jijini London mnamo Desemba 2019.

Kulingana na Dkt Juma, Somalia inahadaa ulimwengu katika jibu lake la hivi karibuni ambapo ilikana madai kuwa imeua maeneo nambari 230,  231, 232  na 233 ambayo Kenya ilikuwa imeweka alama na kusema kuwa yalikuwa ndani ya himaya yake majini.

Hata hivyo, Somalia ilitambua malalamishi ya Kenya. Lakini ikasema kuwa haitambui mipaka ambayo imekuwepo kwa muda wa miaka 40 kulingana na Mkataba wa Anglo-Italia uliotiwa saini mnamo 1964 na kuchora mpaka huo.

Baada ya mkataba huo kutiwa saini makubaliano yalifikiwa katika Mkutano wa Baraza Kuu la Muungano wa Mataifa huru ya Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU) mnamo 1964 ambayo yalidumisha mipaka yote iliyoanishwa wakati wa enzi ya ukoloni.