Habari za Kitaifa

Kenya kuagiza sukari nje ya COMESA

March 31st, 2024 1 min read

NA VICTOR RABALLA

SERIKALI sasa inapania kuagiza sukari zaidi kutoka mataifa yasiyo wanachama wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (Comesa), kufuatia uhaba wa bidhaa hiyo nchini na katika mataifa ya ulimwengu.

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alisema hatua hiyo pia imechangiwa na kupungua kwa uzalishaji miwa nchini mwaka jana — hadi tani 466,000 kutoka 796,000 mwaka 2022.

“Hali hii imesababishwa na madhara ya uwekezaji finyu katika mpango wa kustawisha kilimo cha miwa. Pia kiangazi kilichosababisha uvunaji na usagaji miwa ambayo haikuwa imekomaa,” akasema.

Katika barua aliyomwandikia Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u, Bw Linturi aliomba muda wa kuagiza sukari kutoka nje uongezwe.

“Kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa sukari katika soko la kimataifa, ipo haja ya waagizaji wa bidhaa hii kupewa muda zaidi,” akasema.

Waziri Linturi anataka kibali cha uagizaji sukari, kilichochapishwa kwenye gazeti la serikali – Nambari 14093 ya Oktoba 13, 2023 na Nambari 19358 ya Agosti 9, 2023 – kiongezwe muda hadi Juni 30, 2024.

Alisema ni tani 103, 870 pekee za sukari ziliagizwa chini kwa kibali Nambari 10358, ikilinganishwa na tani 290,000 zilizoidhinishwa.

“Kwa hivyo, kuambatana na kibali hicho tani 186,130 hazikuwasili nchini licha ya stakabadhi hitajika kutolewa,” Bw Linturi alihoji.

Waziri aliongeza kuwa uhaba wa sukari katika mataifa ya ulimwengu yanayoizalisha kwa wingi umechangia kupanda kwa bei yake, na kuathiri gharama ya waagizaji kuileta nchini kwa bei nafuu.

“Kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji sukari nchini, inakadiriwa mwaka huu wa 2024 Kenya itakuwa na uhaba wa tani 194, 000,” akasema.

Hitaji la sukari nchini limefikia tani 1.2 milioni — tani 1 milioni za sukari ya kutumiwa nyumbani na tani 200, 000 za sukari ya viwandani.

Waziri Linturi alisema taifa linahitaji jumla ya tani 720, 000 za sukari kati ya Januari 2024 na Agosti 2024; hitaji litakalotimizwa kwa kuongezea sukari inayoagiza kutoka nje kwa ile inayozalishwa nchini.