Habari Mseto

Kenya kunufaika na mradi wa kuweka intaneti vijijini

December 20th, 2018 1 min read

NA AGGREY MUTAMBO

KENYA ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayotarajiwa kunufaika na mradi mpya unaolenga kupanua idadi ya maeneo ambayo raia wake wanaweza kufikia huduma za mtandao Barani Afrika.

Benki ya uwekezaji ya Bara Uropa, Jumanne ilitangaza kwamba itafadhili kampuni moja ya kibinafsi kujenga miundombinu ya kupenyeza huduma za intaneti katika vijiji vya mashambani nchini Kenya, Rwanda, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mradi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miaka miwili na utatekelezwa na kampuni ambayo jina lake bado halijatangazwa.

Lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha uwezo wa raia wa mataifa hayo kunufaika na huduma za mtandao ili kurahisisha shughuli zao za kiuchumi kupitia njia za kidigitali.

Kulingana na benki hiyo, mradi huo utagharimu Sh1.8bilioni hii ikiwa sehemu ya mabilioni ya fedha yaliyotengewa uimarishaji wa miradi mbalimbali kama uchukuzi, kawi safi na uwezo wa kufikia intaneti barani Afrika.

“Uchukuzi wa kutegemewa, kawi na mitandao ya mawasiliano ni changamoto zinazokabili mataifa ya Bara Uropa na Afrika. Tukifanya kazi pamoja tunaweza kuimarisha maisha ya mamilioni ya watu. Miradi mitatu iliyotiwa saini leo inadhihirisha hili,” akasema Dkt Werner Hoyer, Rais wa Benki ya uwekezaji wa Bara Uropa kupitia taarifa kwa wanahabari Jumanne.

Tangazo hilo lilitolewa pembeni mwa Kongamano kubwa kati ya mataifa ya Bara Afrika na Uropa linaloendelea mjini Vienna, Austria.

Mkutano huo pia unahudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Bara Afrika (AU).

Mada kuu ya Kongamano hilo ni ‘’Kufikisha ushirikiano kwa kizazi cha kidigitali’ na la mno haswa ni kutumia ubunifu na udigitali kama kichocheo cha maendeleo siku zijazo ili kunufaisha kila raia wakati dunia inapoendelea kukumbatia mwamko mpya wa utandawazi.