Habari Mseto

Kenya kuondolea Uchina vikwazo vya kibiashara

November 15th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali itaondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Kenya na China kwa lengo la kukuza kiwango cha bidhaa za Kenya zinazouzwa katika soko la China.

Waziri wa Biashara na Viwanda Peter Munya alisema jopo maalum litakalofanikisha kuondolewa kwa ushuru wa asilimia 4 kwa bidhaa za wauzaji wa Kenya limeundwa.

Hii ni baada ya Wizara ya Kilimo na Idara ya Forodha ya China kutia sahihi mkataba wa makubaliano ambao utawezesha kuuzwa nchini China zaidi ya asilimia 40 mboga, matunda, maua, nyama, korosho na stevia kwa lengo la kupunguza tofauti za kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Munya alisema mkutano wa kwanza utakuwa Januari 2019 na majadiliano yatakamilika Februari 2019.

Alisema hayo wakati wa kuzindua maonyesho ya viwanda kati ya Kenya na China Jumatano.

Maonyesho hayo yanaendelea baada ya kuanza Jumatano na yanatarajiwa kukamilika Jumamosi.

Bidhaa ambazo Kenya huuzia China ni majani chai, kahawa na ngozi ilhali taifa hilo huuzia Kenya bidhaa tofauti kutoka chakula, mashine na teknolojia.

Jopo hilo litajumuisha wataalam wa kibiashara na makatibu wakuu na litaidhinishwa na wizara.