Michezo

Kenya kupigwa marufuku na FIFA kwa kutomlipa Amrouche

April 25th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limetangaza Ijumaa litapatia mataifa 211 ambao ni wanachama wake Sh53.5 milioni kila mmoja kuyasaidia wakati huu kuna janga la ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) huenda lisipate fedha hizo kwa sababu lina deni la kocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouche la Sh109 milioni na linatarajiwa kulilipa kabla ya makataa ya kufanya hivyo ikamilike Aprili 24, 2020.

Amrouche, ambaye ni Mualjeria na pia ana uraia wa Ubelgiji, alinoa Stars kutoka Machi 2013 hadi Agosti 2014 kabla ya kuangukiwa na shoka akiwa bado na kandarasi na Shirikisho la Soka Kenya. Alishtaki Kenya na kushinda fidia hiyo ya mamilioni ya shilingi, ambayo Kenya imekuwa ikijikokota kulipa.

Majuzi, Rais wa Shirikisho la Soka Kenya Nick Mwendwa alisema shirikisho lake halina fedha zozote za kulipa kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 na kuomba serikali iingilie kati, lakini serikali ikataka shirikisho hilo libebe mzigo wake lenyewe.

Fifa imetangaza Ijumaa kuwa fedha inazotokoa kwa mashirikisho wanachama ni za mwaka 2019 na 2020 za kuendesha shughuli zao kama hatua ya kwanza ya mpango wa kupunguzia jamii ya kabumbu mzigo wa athari za ugonjwa huo unaosababishwa na virusi hatari vya corona. Virusi vya corona vimeenea katika mataifa 210 duniani na kusimamisha shughuli za michezo kwa muda usiojulikana. Kenya imethibisha visa 332 vya maambukizi na kuripoti vifo 14.

“Hatua hii inamaanisha kuwa tutatoa karibu Sh16 bilioni kusambazwa kwa mashirikisho 211 kote duniani,” Fifa imesema.

“Janga hilo limeleta changamoto nyingi ambazo hazikuwa zimetarajiwa kwa familia yote ya soka duniani, na kama shirikisho linalosimamia soka ulimwenguni, ni jukumu la Fifa kuwa hapo na kusaidia mataifa yanayohitaji msaada zaidi,” alitangaza Rais wa Fifa, Gianni Infantino.

Aliongeza, “Tunaanza na kutoa usaidizi huu wa kifedha bila kuchelewa kwa mataifa wanachama, mengi yanayokabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha.”