Michezo

Kenya kushiriki vipute vya Cecafa vya kufuzu kwa fainali za AFCON kwa chipukizi wa U-17, U-20

October 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATAIFA 10 yamethibitisha kushiriki mechi za Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 na 20.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati Kuu ya Cecafa, mechi za kufuzu kwa fainali za AFCON U-20 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Novemba 22 na Disemba 6 nchini Tanzania huku zile za U-17 zikipangiwa kutandazwa kati ya Disemba 13-28 nchini Rwanda.

Kwa kila kitengo, timu hizo zitapangwa kwa makundi mawili ambapo vikosi viwili vya kwanza vitafuzu moja kwa moja kushiriki nusu-fainali.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa), Regis Uwayezu, amethibitisha kwamba Rwanda haitashiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za AFCON U-20 mwaka huu wa 2020.

Waandalizi wa mashindano hayo ya Cecafa wanatarajiwa kuandaa droo ya mechi za makundi wiki ijayo mjini Arusha, Tanzania na kutoa pia makataa ya wachezaji, makocha na wasimamizi wa timu husika kufanyiwa vipimo vya corona kabla ya kuingia kambini.

Rwanda almaarufu Amavubi haijawahi kushiriki fainali za AFCON U-17 na U-20 tangu iwe mwenyeji wa fainali za makala ya 2009 na 2011 mtawalia.

Japo chipukizi wa Amavubi U-20 walibanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi mnamo 2011, vijana wao wa U-17 waliduwaza wengi kwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za FIFA zilizoandaliwa nchini Mexico mwaka huo.

Hadi kufikia sasa, Rwanda ndiye mwanachama wa pekee wa Cecafa anayejivunia kuwahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia za FIFA.

Mataifa yatakayoshiriki Cecafa U-17:

Burundi, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Rwanda (wenyeji).

Mataifa yatakayoshiriki Cecafa U-20:

Somalia, Burundi, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Tanzania (wenyeji).