Habari Mseto

Kenya kusutwa na AU kuhusu maskwota wa Mau

January 4th, 2020 1 min read

RICHARD MUNGUTI na JUSTUS WANGA

UHUSIANO wa Kenya na Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) umetiwa doa baada ya Serikali kukaidi agizo la kutofukuza familia 60,000 kutoka kwa msitu wa Mau.

Kunatarajiwa kuwe na mkinzano mkali wakati wa mkutano wa AU pale ambapo Kenya itashtakiwa kukandamiza haki za watu waliofukuzwa msitu wa Mau.

Tume ya kutetea haki za binadamu barani Afrika (ACHPR), imetisha kuishtaki Kenya katika mkutano ujao wa AU.

Tume hiyo mnamo Novemba 2019 iliipa Kenya siku 15 kusitisha hatua ya kuwatimua watu kutoka msitu wa Mau kusubiri kesi iliyoshtakiwa na wahasiriwa.

Tume hiyo iliamuru serikali isitishe kuwatimua watu kutoka msitu wa Mau kwa vile ni ukandamizaji wa haki zao.

Katika barua kwa Rais Uhuru Kenyatta, mwenyekiti wa tume hiyo ya ACHPR Bw Solomon Ayele Dersso alisema kwamba kufukuzwa kwa watu kutoka makazi yao ya Mau ni ukiukaji wa sheria na makubaliano ya mataifa wanachama wa AU kuhusu haki za binadamu.

“Nakuhakikishia kwamba afueni ambayo Kenya ilipewa sio kizingiti cha kutoichukulia Kenya hatua siku za usoni kuhusu suala la kuwatimua watu kutoka msitu wa Mau,” alisema Bw Dersso katika barua aliyomuandikia Rais Kenyatta mnamo Novemba 9, 2019.

Serikali haikuzingatia agizo hilo la ACHPR na mnamo Januari 2, 2020.

Mshirikishi wa Masuala ya Serikali eneo la Rift Valley Bw George Natembeya aliwatahadharisha wahasiriwa dhidi ya kununua mashamba kilomita mraba kutoka msitu wa Mau.

Bw Natembeya alidai wanaowafadhili familia zilizofukuzwa kutoka Mau wanalenga kuhujumu juhudi za Serikali za kuokoa msitu huo ambao ni chemichemi za maji.