Habari Mseto

Kenya kuuza mafuta ng’ambo chini ya mpango wa majaribio

July 24th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

KENYA sasa iko tayari kusafirisha mafuta nje ya nchi kwa mara ya kwanza na hivyo kuweka historia Afrika Mashariki.

Kampuni ya uchimbaji mafuta ya Tullow Oil imesema, kiwango cha mafuta kutoka Turkana kilichofikishwa Mombasa kwa uhifadhi, sasa kimetosha kusafirishwa kwa meli hadi nchi ya kigeni kwa majaribio ya kibiashara.

Mpango huo unatarajiwa kufanikishwa kabla robo hii ya tatu ya mwaka ikamilike Septemba, ingawa haijajulikana wazi mafuta yanasafirishwa hadi nchi gani.

Kwenye ripoti ya kibiashara iliyotumwa kwa wanahabari Jumatano, Tullow ilisema kufikia sasa mapipa 200,000 ya mafuta ambayo ni sawa na lita 31.8 milioni yamehifadhiwa Mombasa.

“Nimefurahishwa zaidi na hatua zilizopigwa Kenya kwani inatarajiwa mafuta yatasafirishwa nje ya nchi hivi karibuni kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa Tullow, Bw Paul McDade.

Tullow ilisema hatua kubwa zilizopigwa sasa zimeleta matumaini kwamba, Kenya itaanza rasmi biashara ya uuzaji mafuta kati ya Julai na Desemba mwaka ujao. Usafirishaji mafuta kutoka Turkana ulikumbwa na vikwazo tele vilivyopelekea mpango wa serikali kuanzisha shughuli hiyo kabla 2017 kugonga mwamba.

Rais Uhuru Kenyatta alizindua usafirishaji kutoka Turkana hadi Mombasa mwaka uliopita, lakini kukawa bado na changamoto hasa kuhusu usalama, miundomsingi na maelewano ya ugavi wa mapato ya rasilimali hiyo kati ya serikali kuu, za kaunti na jamii za maeneo ambako mafuta yanachimbwa.

Tullow jana ilisema mashauriano kuhusu masuala ya kifedha yalikamilika na kupitishwa mnamo Juni 25 mwaka huu, hatua ambayo ilitia moyo kuendeleza mbele mradi huo utakaoingiza Kenya kwenye orodha ya mataifa Afrika yanayojiletea mapato kutoka kwa uuzaji mafuta.

Naibu Msimamizi Mkuu wa kampuni hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki, Bw Mark MacFarlane alisifu ushirikiano ulioshuhudiwa na kusema ulisaidia mno kufanya mradi upige hatua kwa kasi.

“Tumeona jinsi matokeo bora yanaweza kupatikana wakati mashirika yanaposhirikiana kwa karibu na serikali ambako yanaendeleza biashara zao,” akasema.

Mpango wa kudumu ni kujenga bomba litakalosafirisha mafuta kutoka Turkana hadi bandari mpya inayojengwa Lamu.