Kenya Kwanza kufanya mkutano wa kwanza

Kenya Kwanza kufanya mkutano wa kwanza

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Kenya Kwanza umeitisha mkutano wa kwanza wa viongozi wake waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mkutano huo wa magavana, wabunge, wabunge wawakilishi wa kike na maseneta utafanyika katika makazi rasmi ya Rais Mteule William Ruto Jumatano, Agosti 17, 2022.

“Rais Mteule Dkt William Ruto na Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua wanawaalika viongozi waliochaguliwa kuhudumu kama maseneta, wabunge na magavana,” ikasema taarifa ya mwakiliko iliyotumwa kwa viongozi hao na Katiba Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Veronica Maina.

“Mkutano huu utafanyika katika makazi ya Naibu Rais mnamo Jumatano Agosti 17, 2022 saa tatu za usubuhi,” Bi Maina akasema.

Katibu huyo Mkuu wa UDA pia alisema kuwa Dkt Ruto na Bw Gachagua wataongoza mikutano ya kwanza ya madiwani wote waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza.

Jumla ya maseneta 24 walichaguliwa kwa tiketi za vyama vilivyo ndani ya Kenya Kwanza dhidi ya viti 23 ambavyo muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya umepata.

Azimio ilipata idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa baada ya kushinda viti 162 ikilinganishwa na viti 159 ambavyo Kenya Kwanza ilipata.

Kwa upande wa magavana muungano wa Kenya Kwanza ulishinda viti 22 huku Azimio ikishinda viti 23, kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Mombasa na Kakamega.

  • Tags

You can share this post!

Hesabu yakanganya makamishna walioasi matokeo ya urais

NJENJE: Mapato ya uuzaji mboga na matunda yashuka,...

T L