Kenya Kwanza yaanza kutikiswa na mivutano

Kenya Kwanza yaanza kutikiswa na mivutano

DALILI zimeanza kuibuka katika muungano tawala wa Kenya Kwanza, zikionyesha unakumbwa na mzozo wa ndani, miezi miwili pekee baada ya kuingia madarakani.

Hali hii imejitokeza baada ya viongozi wake kuanza kutofautiana kuhusu maamuzi muhimu, yakiwemo ya kiserikali, hasa kuhusu uteuzi wa wawakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), uagizaji wa mahindi yaliyobadilishwa maumbile kisayansi (GMO) na ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi.

Mvutano unaotokota unahusisha zaidi washirika wakuu katika muungano huo, ambao ni viongozi kutoka ngome ya Rais William Ruto ya Rift Valley na wale wa kutoka ngome ya naibu wake Rigathi Gachagua ya Mlima Kenya.

Tukio la majuzi ni vitisho vya wabunge kutoka Rift Valley vya kuwasilisha mswada bungeni wa kumtimua Waziri wa Biashara, Moses Kuria kwa mpango aliotangaza majuzi wa kuagiza magunia 10 milioni ya mahindi ya GMO.

Wabunge hao wanasema mpango huo ni hujuma kwa wakulima katika maeneo yao, ambao kwa sasa ndio wanavuna mahindi.

“Mahindi ya GMO yatafurika sokoni na kuathiri bei ya mahindi ya wakulima wa humu nchini, ikizingatiwa gharama ya kilimo iko juu,” akasema Seneta Samson Cheragei wa Nandi kwenye taarifa kwa niaba ya viongozi wenzake.

Mvutano kuhusu Bw Kuria ulitanguliwa na hatua ya wabunge wa Mlima Kenya wiki jana kumkaidi Rais Ruto wakati wa uchaguzi wa wawakilishi wa Kenya katika EALA.

Wakati wa uchaguzi huo, Bw Gachagua alikiri kwamba aliongoza wabunge kutoka Mlima Kenya kukaidi agizo la Rais Ruto kuhusu orodha ya wanachama wa Kenya Kwanza katika bunge hilo la kanda.

Bw Gachagua alisema alikuwa msitari wa mbele kuweka mikakati ya kuhakikisha eneo la kati lilikuwa na waakilishi katika EALA, na akatangaza wazi kuwa alimsaidia aliyekuwa mbunge wa Kieni, Kanini Kega wa muungano wa upinzani wa Azimio kuchaguliwa na wabunge.Wabunge hao wa Mlima Kenya walikaidi chaguo la Rais Ruto kumchagua Fred Muteti, na badala yake wakampigia kura Mwangi Maina, ambaye hakuwa kwenye orodha ya Kenya Kwanza iliyoidhinishwa na rais.

Siku iliyofuata, Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga, alisema kuungana kwa wabunge wa Mlima Kenya kumchagua Bw Kega ilikuwa ni onyo kwa muungano tawala wa Kenya Kwanza kwamba eneo hilo haliwezi kulazimishwa kufanya mambo.

“Safari hii tutatembea pamoja au tunaweza kusema ikiwa hatutakiwi kwenda pamoja. Hatujaolewa na mtu mmoja anayeweza kututawala kisiasa. Tuligundua baadhi ya watu wanajaribu kucheza nasi kisiasa. Ndio maana tulimchagua Kanini Kega. Tutaendelea kuwachagua watu wetu. Bado ni mapema katika mbio hizi,” Bw Kahiga alisema kuhusu eneo la Mlima Kenya kusalia Kenya Kwanza.

Hapo jana Jumatano Bw Kega alimsifu Bw Gachagua kama kiongozi wa eneo la Mlima Kenya, akisema kuna haja ya eneo hilo kusimama nyuma yake.

Ingawa Bw Gachagua amesisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya liko nyuma ya Rais Ruto, tofauti zinazoibuka zinaashiria kuna mgawanyiko katika maamuzi unaotokota.

Duru zinasema kwamba kutokana na tofauti katika muungano huo, Bw Mudavadi hajapata ofisi za kuhudumu huku alizotengewa katika jengo la Shirika la Reli la Kenya zikiendelea kukarabatiwa.

Wasaidizi wa Bw Mudavadi, ambao hawakutaka tutaje majina yao, walisema kumekuwa na mvutano kati ya makamu rais huyo wa zamani na Bw Gachagua uliofanya asiingie ofisi za muda katika jumba la Treasury.

Mivutano ambayo imeanza kuandama Kenya Kwanza inaendeleza mtindo ambao umekuwa ukishuhudiwa nchini kila mara miungano ya kisiasa inapochukua madaraka, ambapo viongozi walioungana kushinda wamekuwa wakifarakana.

Mnamo 2002, migawanyiko mikubwa ya kisiasa na sera iliandama muungano ulioongozwa na Mwai Kibaki wa Narc, ambao hatimaye ulisambaratika baada ya mrengo mmoja kutimuliwa serikalini mnamo 2005.

Kwa miaka mitano tangu 2018, mvutano mkali kati ya Rais Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ulitawala kipindi cha mwisho cha utawala wao chini ya muungano wa Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

Galana-Kulalu kukabidhiwa wawekezaji wa kibinafsi

TAHARIRI: GMO: Serikali ielimishe wananchi kuondoa dukuduku

T L