Kenya Kwanza yataka kampuni za Uhuru zianze kulipa ushuru

Kenya Kwanza yataka kampuni za Uhuru zianze kulipa ushuru

NA COLLINS OMULO

BAADHI ya maseneta wa Kenya Kwanza sasa wanaitaka serikali ishurutishe familia ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta (pichani) kulipa ushuru.

Maseneta hao wanataka ukaguzi dhidi ya ushuru ambao familia hiyo haijalipia mashamba yake yaliyozagaa kote nchini.

John Methu (Nyandarua), James Murango (Kirinyaga), Wahome Wamatinga (Nyeri) na Seneta Maalum Tabitha Mutinda walidai kuwa Bw Uhuru ndiye anayefadhili mikutano ya Azimio la Umoja-One Kenya inayoendeshwa na Raila Odinga.

“Kila mtu lazima alipe ushuru. Kulipa ushuru ni wajibu wa kitaifa na yeyote anayewachochea watu wasilipe ushuru si mzalendo,” akasema Bw Methu.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Rais William Ruto akiwa mjini Mombasa, ambapo alimlaumu mtangulizi wake kwa kutolipa ushuru na kutumia mali yake kudhamini ghasia dhidi ya utawala wake.

“Kila mmoja wetu lazima alipe ushuru. Hatuwezi kuendelea na hali ambapo, wale walio katika mamlaka wanajiepusha kulipa ushuru. Wanatumia kila mbinu kuhepa, huku wasio na uwezo wakilipa. Ninachosema ni kuwa, wale waliozoea kukwepa mzigo wa kulipa ushuru, mwisho wao umefika. Kila mwananchi lazima alipe ushuru,” akasema.

Rais alidai kuwa hata watu hao wakifadhili maandamano ili wasilipe ushuru, hawatafaulu kwa hilo.

  • Tags

You can share this post!

Real Madrid wakabwa koo na Sociedad katika La Liga ugani...

Napoli watandika AS Roma na kufungua pengo la alama 13...

T L