Michezo

Kenya Lionesses roho juu baada ya idadi ya washiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2025 kuongezwa

December 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Lionesses, kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia sasa yako hai.

Hii ni baada ya Shirikisho la Raga Duniani (WR) kuongeza idadi ya washiriki wa makala yajayo ya fainali hizo mnamo 2025 kutoka 12 hadi 16.

Bara la Afrika ambalo kwa kawaida limekuwa likitengewa tiketi moja ya uakilishi wa moja kwa moja (direct ticket), sasa litakuwa na nafasi mbili, jambo ambalo linatazamiwa kutia Lionesses katika nafasi bora zaidi ya kufuzu kwa mashindano hayo ya haiba kubwa duniani.

“Maamuzi hayo, ambayo yamechukuliwa na Bodi ya Usimamizi wa Kombe la Dunia, ni ishara kubwa kuhusu jinsi WR ilivyojitolea kuchangia makuzi ya raga ya wanawake duniani na kufanikisha baadhi ya mipango-mikakati yake ya mwaka 2017 hadi 2015,” ikasema sehemu ya taarifa ya shirikisho hilo.

Meneja wa timu ya Lionesses, Camilyne Oyuayo amepokea vyema maamuzi ya WR kupanua zaidi ushiriki wa fainali zijazo za Kombe la Dunia na ni mwingi wa matumaini kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa nchi ndogo zinazoinukia kwenye mchezo kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao kwenye ulingo wa raga ya kimataifa.

“Ni nafasi nzuri itakayochangia makuzi ya wachezaji wetu na viwango vya mchezo wa raga kwa ujumla. Hii ni fursa njema kwa Kenya kunogesha fainali hizo. Ni jambo litakalowezekana iwapo tutaimarisha miundo-msingi yetu na kuboresha zaidi vigezo tunavyotumia kutafuta vipaji vya raga mashinani,” akasema Oyuayo.

Lionesses wangali katika vita vya kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazondaliwa nchini New Zealand mnamo 2021 baada ya mchuano wao wa kufuzu dhidi ya Colombia kuahirishwa mapema mwaka huu kutokana na janga la corona.

Kwa mujibu wa Oyuayo, mechi hiyo kwa sasa huenda ikachezewa uwanjani RFUEA mnamo Aprili 2021. Iwapo Lionesses watabwaga Colombia, basi watafuzu kwa raundi ya mwisho wa mechi za kufuzu ambapo watakutana na wapinzani kutoka bara Ulaya na Asia mnamo Juni mwakani.

Iwapo watatia fora katika hatua hizo za mwisho, basi watajikatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza ambapo watakutanishwa na Wales, Australia na wenyeji New Zealand ambao pia ni mabingwa watetezi.

Lionesses walikosa kupata tiketi ya moja kwa moja ya kuwakilisha Afrika kwenye fainali hizo za 2021 baada ya kudhalilishwa 39-0 na Afrika Kusini jijini Johanesburg mnamo 2019.

Oyuayo amesema Lionesses kwa sasa wanajivunia motisha ya kiwango cha juu kadri wanavyojiandaa kuanza mazoezi kwa minajili ya mechi dhidi ya Colombia mwakani.

Wakati uo huo, timu ya taifa ya wanaume ya wanaraga saba kila upande almaarufu Shujaa, imepata mwaliko wa kucheza nchini Uhispania na Ufaransa mnamo Februari 2021, mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kampeni za duru ya Raga ya Dunia.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Oduor Gangla amethibitisha kwamba wamepata mwaliko huo kutoka Uhispania na Ufaransa na ameeleza matumaini kwamba vipute hivyo vitakuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Shujaa kwa muhula mpya.

“Mashindano ambayo tumealikwa kushiriki katika mataifa hayo yatapiga jeki maandalizi ya Shujaa kwa minajili ya Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande na michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan mnamo Julai 2021,” akasema Gangla.

Mbali na Kenya, vikosi vingine ambavyo vimealikwa kwa vipute hivyo nchini Uhispania na Ufaransa ni New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa.

Kwa mujibu wa Gangla, washindani wa Shujaa katika vipute vya Raga ya Dunia na Olimpiki wamekuwa wakiendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mapambano mengine muhimu – jambo ambalo timu ya taifa inafaa pia kuanza kufanya.

“Hatuwezi kuendelea kukaa na kusubiri kwa sababu tuko nyuma ya ratiba. Washindani wetu wanafanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali katika mataifa yao,” akahoji Gangla.