Michezo

Kenya Lionesses tayari kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia

August 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Lionesses imejawa na matumaini makubwa itatikisa kwenye mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande ya wanawake yatakayofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini mnamo Agosti 9-17, 2019.

Akitaja kikosi chake cha mwisho Alhamisi, kocha Felix Oloo alisema, “Tumekuwa tukipiga msasa idara tulizoona kuna ulegevu wakati wa Elgon Cup na pia kuhakikisha kila mchezaji anafahamu majukumu yake kwenye timu. Tumekuwa na kambi ya mazoezi na tuna matumaini kuwa timu iliyochaguliwa itafanyia Kenya kazi nzuri.”

Mchezaji Sheila Chajira amerejea kikosini baada ya kukosa mechi mbili zilizopita dhidi ya Uganda kwenye raga ya Elgon Cup zilizosakatwa Juni 22 mjini Kisumu na Julai 13 mjini Kampala.

Alikuwa nje akiuguza jeraha la kifundo alilopata dhidi ya Brazil katika mechi ya nusu-fainali ya mashindano ya kufuzu kushiriki Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande ambayo Kenya ilipoteza mjini Hong Kong mwezi Aprili.

Uzoefu wake katika mashindano ya kimataifa utaongeza nguvu katika timu ya Kenya. “Nafurahia sana kurejea katika kikosi kitakachoshindania tiketi ya kuingia Kombe la Dunia. Nimekuwa nikihudhuria mazoezi nikipata afueni na nimejawa na imani tutafanya vyema,” alisema Chajira.

Lionesses ilirarua Lady Cranes ya Uganda 44-13 mjini Kisumu na kuilima 33-5 mjini Kampala na kutwaa taji la Elgon Cup kwa jumla ya alama 77-18. Ilitumia mechi hizo pia kujipima nguvu.

Oloo pia amejumuisha katika kikosi chake wachezaji wapya kabisa Vivian Akumu na Naomi Amuguni. Walivutia sana katika mazoezi.

Lionesses, ambayo ilishinda Kombe la Afrika la wachezaji saba kila upande kwa mara yake ya kwanza kabisa mwaka 2018, itaanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la wachezaji 15 kila upande dhidi ya wanavisiwa wa Madgascar mnamo Agosti 9.

Kisha, Lionesses itavaana na Lady Cranes mnamo Agosti 13 na kukamilisha kampeni yake dhidi ya miamba Afrika Kusini mnamo Agosti 17.

Mshindi wa mashindano haya ya kufuzu itaingia Kombe la Dunia litakalofanyika nchini New Zealand mwaka 2021.

Nambari mbili atapata fursa ya mwisho ya kupigania tiketi dhidi ya timu kutoka Amerika Kusini.

Kikosi cha Kenya Lionesses:

Juliet Nyambura (Northern Suburbs), Imogen Hooper (Northern Suburbs), Everlyne Kalimera (Stanbic Mwamba), Mercy Migongo (Menengai Cream Homeboyz), Knight Otuoma (Kisumu), Staycy Atieno (Stanbic Mwamba), Victoria Gichure (Northern Suburbs), Millicent Opala (Menengai Cream Homeboyz), Bernedatte Oleisia (Menengai Cream Homeboyz), Enid Ouma (Menengai Cream Homeboyz), Emmaculate Owiro (Menengai Cream Homeboyz), Michelle Akinyi (Impala Ladies), Leah Wambui (Menengai Cream Homeboyz), Janet Owino (Menengai Cream Homeboyz), Naomi Amuguni (Stanbic Mwamba), Irene Atieno (Menengai Cream Homeboyz), Veronicah Wanjiku (Top Fry Nakuru), Vivian Akumu (Top Fry Nakuru), Grace Adhiambo (Top Fry Nakuru), Philadelphia Orlando (Northern Suburbs), Celestine Masinde (Stanbic Mwamba), Sheila Chajira (Menengai Cream Homeboyz), Diana Awino (Impala Ladies), Stella Wafula (Impala Ladies), Christabel Lindo (Impala Ladies), Janet Okelo (Stanbic Mwamba).

Ratiba:

Agosti 9

Madagascar na Kenya

Afrika Kusini na Uganda

Agosti 13

Kenya na Uganda

Madagascar na Afrika Kusini

Agosti 17

Madagascar na Uganda

Afrika Kusini na Kenya