Michezo

Kenya Lionesses yapata mshauri wa hali ya juu Peter Harding kwa ajili ya Olimpiki, Kombe la Dunia

December 11th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAURI wa mazoezi ya hali ya juu ya kuimarisha mchezo wa wachezaji na timu, Peter Harding amejiunga na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) kwa mkataba wa miezi mitatu kusaidia kuimarisha timu za taifa.

Katika majukumu yake, Harding, ambaye amependekezwa kwa Kenya na Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby), atasaidia KRU kuandaa timu zake, hasa ile ya taifa ya wanawake ya wachezaji saba kila upande almaarufu Kenya Lionesses kwa michezo ya Olimpiki 2020. Olimpiki itafanyika kutoka Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka 2021 jijini Tokyo nchini Japan baada ya kuahirishwa kutoka mwaka 2020 kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Harding pia atasaidia timu ya wanawake ya wachezaji 15 kila upande inaporejelea mazoezi na maandalizi ya mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2021 dhidi ya Colombia.

Jukumu lake lingine ni kuunda na kusimamia mipango ya mchezo wa timu za Kenya kuanzia sasa na kuendelea.

Harding ni mtaalamu wa masuala ya viwango vya juu vya ukufunzi ambaye amefanya kazi na timu nyingi za taifa na wanamichezo kwa zaidi ya miaka 25.

Kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita, amejihusisha na mchezo wa raga pekee akitwikwa majukumu ya mkuu wa mazoezi ya kuimarisha mchezo wa wachezaji na timu wa wanaraga wa Uingereza pamoja na timu ya Australia almaarufu kama Wallabies kwa muhula mzima wa Kombe la Dunia.

Majukumu ambayo amefanya hivi majuzi ni ya Mkurugenzi Mkuu wa timu za taifa za Tonga na Namibia katika masuala ya mazoezi ya hali ya juu na pia ameshauri World Rugby kuhusu miradi mbalimbali ikiwemo kufanya kazi na timu anayopenda, Lionesses.

Akizungumzia kazi yake mpya, Harding alisema anafurahia kutoa msaada wowote anaoweza.

“Kenya ina timu mbili zilizo na viwango vya kimataifa ambazo zitashiriki Olimpiki mwaka 2021, timu ya wachezaji 15 kila upande ina fursa ya kuingia Kombe la Dunia na kisha mwaka utakaofuata timu ya wanaume ya wachezaji 15 kila upande kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia. Ni wakati wa kuamini kuwa kuna fursa ya kweli ya KRU kuonekana kwenye ramani ya dunia ya raga sio tu katika raga ya wachezaji saba kila upande, bali pia ile ya wachezaji 15 kila upande,” akasema.

Mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla alielezea furaha ya kuja kwa Harding kama mshauri wa masuala ya mazoezi ya hali ya juu.

Harding si mgeni Kenya kwani aliwahi kufanya kazi na Lionesses kabla ya Olimpiki 2016 zilizofanyika nchini Brazil ambapo Lionesses ilizoa matokeo kadhaa mazuri.

“Ujuzi wake wa kufanya kazi na mataifa yanayoinuka katika mchezo wa raga ambayo yamecheza katika viwango vya juu, utasaidia raga ya Kenya kufikia viwango vipya kupitia kuboresha mafunzo ambayo makocha wetu wamepata. KRU pia inashukuru msaada wa mara kwa mara kutoka kwa World Rugby na Shirikisho la Raga Afrika (Rugby Africa) ambao wamefanikisha mshauri wa kiwango cha juu kuja hapa na aliye na ujuzi wa kusaidia KRU.” Mkataba wa Harding unaweza kuongezwa baada ya kukamilika.