Habari za KitaifaUncategorized

Kenya mbioni kuhakikisha Raila anapata ungwaji kutoka wanachama wa EAC


KENYA sasa inaziomba nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimuidhinishe Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kama mwaniaji wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kutoka ukanda huu.

EAC ina mataifa manane wanachama ambayo ni Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania. Makao makuu ya EAC ni Arusha, Tanzania.

Bw Odinga Jumapili alikuwa anatarajiwa kuhutubia Kongamano la Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni kutoka EAC. Kongamano hilo ambalo lilianza Jumamosi liliandaliwa Zanzibar na linakamilika leo Jumatatu.

Ukitamatika, mawaziri wa nchi za kigeni kutoka EAC wanatarajiwa kutangaza kwa kauli moja kuwa watavumisha azma ya Bw Odinga katika mataifa mengine.

Wiki jana, Bw Odinga aliandaa mkutano na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit kule Juba ambapo kiongozi huyo alikubali kuunga azma yake.

“Nilikuwa na mkutano uliofana mno wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit. Nathamini na kumshukuru kwa kukubali kuniunga mkono na kupeleka ujumbe huo kwa mataifa ya EAC,” akasema Bw Odinga baada ya mkutano huo uliofanyika mnamo Alhamisi.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni anaongoza wajumbe kutoka Kenya katika kongamano hilo nchini Zanzibar ambapo Raila anatarajiwa kutoa hotuba yake leo.

“Raila atakutana na mawaziri wa Mashauri ya Kigeni Afrika Mashariki. Atawasikiza na kufahamu changamoto ambazo wanapitia hasa katika uhuru wa kibiashara na utangamano,” akasema Balozi wa zamani wa Kenya Marekani Elkanah Odembo.

Bw Odembo ndiye mkuu wa kitengo cha upangaji wa mikakati katika kikosi cha kampeni cha Bw Odinga. Wengine ni aliyekuwa Naibu Gavana wa Nyeri Dkt Caroline Karugu, Profesa Makau Mutua na Mahboub Maalim.

Bw Odinga anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Ushelisheli Vincent Meriton na waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni kutoka Somalia Fawzia Yusuf.

Wiki jana, Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni Dkt Korir Sing’oei aliandaa mkutano wa kamati ya kiufundi ambayo ilishirikisha kikosi cha Bw Odinga na wale wa serikali. Mkutano huo ulilenga kuweka mipango ya kuwasilisha stakabadhi za kiongozi huyo wa upinzani kwa AU.